Sambaza....

Vitu vingi viliongelewa sana , na kitu kikubwa ambacho kilikuwa kinazunguka katika vinywa vya watu wengi na kauli ya Jurgen Klop. Kauli ambayo aliitoa kipindi ambacho Manchester United wamemnunua Paul Pogba.

Hakutaka kuamini kama soko la mpira wa miguu limefikia hatua ya klabu kutoa pesa kubwa kwa ajili ya kununua mchezaji.

Pesa ambazo ni bajeti kwa timu ambayo inajali vipaji halisi vya wachezaji. Ndiyo utamaduni wake ambao ameishi nao kwa muda mrefu tangu akiwa Ujerumani.

Aliamini katika kuibua vipaji kuliko kutumia pesa kubwa kwa ajili ya kununua kipaji kikubwa.

Kwake yeye aliamini jicho makini linaweza kutafuta mchezaji bora ambaye atakuzwa katika mazingira ya kuwa maradufu zaidi.

Akiwa Ujerumani hakuwahi kabisa kuwa muumini wa kutumia pesa ndefu kwa ajili ya kusajili mchezaji.

Ndiyo maana aliijenga Borrusia Dortmund tishio kwa kutumia vijana wenye vipaji ambavyo vilikuwa havijawahi kuonekana awali.

Aliviamini vipaji hivo, akavipa nafasi kubwa sana na kuamini kuwa vinaweza kufanya vitu vikubwa kama vikijituma kwa ajili ya kutafuta mafanikio binafsi na mafanikio ya timu kwa ujumla.

Ndicho kitu alichofanikiwa kukipata, aliipata Borrusia Dortmund aliyokuwa anaitaka. Borrusia Dortmund tishio iliyotokana na bajeti ndogo sana.

Borrusia Dortmund ilikuja kutingisha utawala wa Bayern Munich.

Keita and Djik

Hatimaye Bundesliga ikawa siyo ligi ya timu moja tena kama ilivyokuwa imezoeleka awali.

Bayern Munich ikawa inaiogopa Borrusia Dortmund, Borrusia Dortmund ikawa inajivunia utawala wake mpya.

Utawala ambao ulihamia mpaka kwenye ligi ya klabu bingwa barani ulaya. Borrusia Dortmund ikawa timu tishio , ukawaida ikawa umeondoka ndani ya klabu ya Borrusia Dortmund.

Kila timu iliihofia Borrusia Dortmund, heshima ikawa juu ya Jurgne Klopp na Gengen Pressing style yake.

Jurgen Klopp alijivunia mafanikio yaliyokuwa kwenye mikono yake. Mikono yake ikawa imepata kiburi kuwa inaweza kutengeneza kitu imara na bora kwa kutumia kiasi kidogo cha pesa.

Hakutaka kabisa kuiaminisha akili yake kuwa utumiaji wa pesa nyingi kwenye usajili unaweza kukupa timu imara na bingwa.

Utampindua vipi akili yake wakati tayari alikuwa na kombe la ligi ya Ujerumani mikononi mwake?

Ilikuwa ngumu sana kumwaminisha kitu tofauti akili mwake wakati ambao macho yake yalishuhudia timu yenye bajeti ndogo ikibeba kombe mbele ya timu yenye bajeti kubwa.

Aliamini katika utafutaji wa vipaji imara, aliamini katika matumizi ya muda ya kutafuta vipaji bora kuliko matumizi ya pesa nyingi ndiyo maana akawa mpingaji mkubwa wa Mino Raiola.

Haya ndiyo maisha yake aliyoyaishi kwa kuyaamini. Hata alipokuja Liverpool aliamini kupitia hilo ndiyo maana alishangazwa na kitendo cha Manchester United kumsajili Paul Pogba kwa kiasi kikubwa cha pesa.

Alisema sana, akazodoa sana na akashangazwa sana lakini mwisho wa siku na yeye aliingia kwenye mtego wa biashara ya mpira wa sasa.

Ikamlazimu kuingia mfukoni kuimarisha safu yake ya ulinzi. Aliamua kupingana na mawazo yake.

Hakuwa na muda tena wa kumtengeneza beki imara na bora wa kati kama alivyowahi kumtengeneza Mats Hummel’s pale Borrusia Dortmund.

Hakuwa na mkono wa birika tena, mfuko ulimtoboka haswa kumnasa Van Djik. Beki ambaye alikuja kutibu matatizo ambayo Liverpool walikuwa nayo.

Liverpool hawakuwahi kuwa na tatizo la ufungaji hata siku moja, ili iliwahi kuwa na tatizo la kulinda kila goli ambalo walikuwa wanalifunga.

Kilikuwa ni kitu cha kawaida kwa Liverpool kushinda magoli 5 kwa 3, kwa sababu walikuwa na safu imara ya ushambuliaji na safu mbovu ya ulinzi.

Ndiyo maana Jurgen Klopp alikuwa anashinda mechi tu na kushindwa kushinda ubingwa.

Kitu hiki kilimuumiza kichwa sana, akaamua kuyalamba matapishi yake kwa kumsajili mchezaji kwa gharama ambayo awali ilimshangaza sana.

Bei ambayo mpaka sasa hajutii kuitoa kwa sababu mchezaji aliyefanikiwa kumleta ndiye mchezaji ambaye alileta uhai katika kikosi cha Liverpool.

Timu ikaimarika, makosa binafsi kwenye safu ya ulinzi yakapungua kwa kiasi kikubwa. Kila MTU akaiona Liverpool iliyokamilika, Liverpool ambayo ilikuwa na uwezo wa kuchukua ubingwa. Na inawezekana Van Djik alikosekana muda mrefu kuitoa njaa ya Liverpool ya kukaa miaka 28 bila ubingwa.

Leo hii wameshinda mechi nne, mechi ambazo wameruhusu goli moja tena goli la kitoto Lililosababishwa na utoto wa golikipa Allison.

Liverpool kwa sasa ni timu imara nyuma na timu tishio mbele na imekamilika ipasavyo katika eneo la katika baada ya ujio wa Naby Keita.

Liverpool imekuwa tofauti na ya misimu miwili iliyopita ambapo katika msimu wa mwaka 2016/2017 na msimu wa mwaka 2017/2018 iliruhusu goli katika mechi za ufunguzi.

Lakini Liverpool hii ya sasa ikikifunga unapata mawazo ya namna gani unaweza kusawazisha kwa kifupi Liverpool hii ni Liverpool ambayo inakuwazisha jinsi ya kuwazuia washambuliaji wake na jinsi ya kuipita ngome yake ya ulinzi.

Inawezekana sifa nyingi anaweza kupewa Naby Keita, lakini ukweli ni kwamba Naby Keita amekuja kukamilisha kazi kubwa ambayo ilifanywa na Van Djik kuanzia msimu uliopita.

Sambaza....