Klabu zinazoendeshwa kisasa huwa zina utaratibu wake maalumu wa kumpa kocha mkataba wa kuifundisha timu kama kocha mkuu au meneja.
Mchakato wa kumpata kocha, huwa ni wa kisayansi unahakikisha kocha anayepatikana anakidhi vigezo wa kuwa kocha mkuu na hata kuiwezesha timu kupiga hatua nyingi mbele.
Kocha akishapatikana, kabla ya kupewa mkataba rasmi kwanza hukabidhiwa mahitaji ya timu. Katika mahitaji hayo timu itaeleza kiundani inataka nini kutoka kwa kocha huyo, ‘target’ za klabu kwa msimu husika, mwisho kabisa klabu itamuuliza kocha huyo kama ataweza kufikia malengo ya klabu kiujumla.
Kocha atajibu,NDIO AU HAPANA.. kama ni ndio kocha naye ataiachia bodi ya wakurugenzi au viongozi vitu ambavyo anavihitaji kukamilishia malengo hayo, ikiwemo wachezaji anaowataka na vingine.
Mchakato huo wa makubaliano ukishapita, kocha hupewa mkataba, mkataba ambao huishi kutokana na matokeo ya makubaliano kwa maana kocha akishindwa kutimiza malengo ya timu hali ya kuwa amepewa kila kitu, basi klabu inaweza kumuacha kocha huyo pia hii hutegemea na masharti ya kimkataba baina ya pande hizi mbili.
SIMBA NA YANGA.
Simba na Yanga ndio roho ya nchi, kwa maana Historia ya nchi katika soka iko mikononi mwa vilabu hivi viwili. Kiukweli vilabu hivi ni vikubwa, tena sana na hata mifumo yake ya kiuendeshaji, vuguvugu kutoka kwa mashabiki, na kutimua za makocha ni sawa na vilabu vikubwa vya barani Ulaya kama Chelsea, Man U na hata Real Madrid.
Kwa mfano Klabu ya Chelsea ndani ya miaka 10 imebadili makocha mara sita, yaani kuanzia kwa Carlo Ancelotti mwaka 2009 hadi kwa Frank Lampad hii ni sawa kwa Manchester United baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.
Karibu katika uchambuzi wa kina juu ya makocha wa Simba na Yanga. Ndani ya makala hii utapata kujua kiundani malengo na mahitaji ya timu kwa kocha husika yaani Simba inataka nini kutoka kwa Aussems na Yanga inataka nini kutoka kwa Zahera.
Msingi mkubwa wa uchambuzi huu ni kuonyesha gharama za klabu za msimu, malengo ya klabu, wapi yanaweza kufanikiwa na wapi yanaweza kukwama kiasi cha kusababisha kocha kutimuliwa.
KANUNI YA ‘WIN/WIN OR NO DEAL’
Miongoni mwa kanuni za msingi za kibiashara ni ile ya WIN/WIN OR NO DEAL. Kanuni hii inasema kuwa ili mapatano yafanikiwe sharti kila upande ulidhishwe na matokeo na uhisi kama umefanikiwa! kinyume na hapo kusiwe na Biashara.
Kwa lugha ya kimombo ni sawa na kusema ‘in a successful negotiation both parties are full satisfied with the result and feel that they have each won or no deal should be made at all’.
SIMBA NA AUSSEMS
Simba ni miongoni mwa vilabu vilivyojizolea umaarufu mwingi sana barani Afrika baada ya Msimu uliopita kufika hatua ya Robo fainali klabu bingwa Afrika.
Kutokana na mafanikio hayo waliyoyafikia msimu uliopita, yaliwasukuma kuongeza bajeti kuwa kubwa zaidi ili msimu huu waweze kuvuka hatua ya robo fainali.
Kufika nusu fainali, na kuchuana na vilabu vikubwa kama TP Mazembe, Al ahly na Wydad Casablanca ndiyo yalikuwa malengo ya klabu. Klabu ilitenga bajeti kubwa ili kuhakikisha Simba inachukua kila kombe itakayoshiriki kuanzia mapinduzi hadi ligi kuu lakini lengo kuu lilikuwa ni kuiona Simba ikivuka hatua ya Robo fainali klabu bingwa Afrika.
Simba ikatolewa hatua ya mchujo na Wamakonde kutoka Msumbiji UD DO Songo na kukatisha ndoto za Mnyama kufika nusu fainali klabu bingwa Afrika licha ya uwekezaji mkubwa walioufanya.
BAJETI YA SIMBA.
Simba inakadiliwa kutenga zaidi ya bilioni 6 kwa ajili ya msimu mzima. Bajeti ambayo imeanza kutumika wakati Simba ikiwa kambini nchini Afrika ya kusini.
Kama unavyojua utengaji wa bajeti, huhusisha makadilio ya fedha zitakazotumika na vyanzo vya mapato vya kupata pesa hizi. Moja ya vyanzo vikuu vya mapato kwa klabu ilikuwa ni mechi za ligi ya mabingwa Afrika.
Klabu ilitengeneza pesa nyingi kutokana na idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa wakijitokeza uwanjani kuishabikia, lakini sasa chanzo hicho kimeshakufa.
Mwisho kabisa, kila hatua klabu itakayopiga katika mnashindano ya kimataifa chini ya Caf, Shirikisho hilo hutoa fedha kwa klabu kama zawadi. Fedha hizi nazo zimeshashindikana. Kiujumla bajeti ya Simba imeshaharibika, kwani makadilio ya wapi bilioni 6 zitapatikana yameharibika.
MKATABA WA AUSSEMS.
Aussems ana mkataba wa mwaka mmoja pekee. Mkataba huo ameongezewa katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili, mkataba huu utamuweka ndani ya Msimbazi hadi mwezi Juni Mwakani.
Vilabu vingi duniani hushindwa kuvunja mikataba na makocha wake kutokana na gharama za kufanya hivyo. Unakuta kocha amebakiza miaka mitatu kumaliza mkataba, kwahiyo klabu huona kuvunja mkataba wa aina hiyo ni hasara kubwa.
Mkataba wa Aussems ni rahisi kuuvunja, na hata wasipouvunja utaisha mwisho wa msimu. Hii ina maanisha kuwa, Aussems anatakiwa kuishawishi bodi ya Wakurugenzi wa Simba kumpa mkataba mpya. Kwa hili ni rahisi sana kumkosa Aussems msimu ujao.
USAJILI ‘BAB KUBWA’ WA SIMBA.
Nani anasema kuwa Simba imefanya usajili mbovu? Simba ina wachezaji bhana. Ukweli ni kwamba klabu hiyo ilidhamilia kufanya kweli kimataifa ndio maana imeshusha mashine za kazi.
Kwa usajili huu, maana yake Simba inatakiwa isiponyokwe na kikombe hata kimoja. Kufanya hivyo ndio pona ya Aussems.
Baada ya kutolewa klabu bingwa Afrika wachezaji wake hawatokuwa na uchovu mwingi wa kucheza mechi nyingi badala yake watawaza mashindano mengine ya nyumbani hivyo lazima wabebe vikombe vyote hata Mapinduzi.
Kwa Usajili huu Aussems hana cha kupoteza zaidi ya kuwa bingwa wa kila kona, kushindwa kufanya hivyo basi msimu ujao hatutokuwa naye.
Tukirudi kwa upande wa Yanga mambo sio magumu sana kiasi cha kushitua japo nako kuna vugu vugu lake.
Msimu uliopita Mashabiki wengi wa Yanga walimpa kongole za dhati kocha wao, Mwinyi Zahera kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kwa kufika nusu fainali kombe la Azam na kushika nafasi ya pili ligi kuu Tanzania bara licha ya ukame uliokuwa ukiikabili timu. Zahera alionekana kuwa bonge la kocha.
NGUVU YA WANANCHI.
Msimu huu mambo ni tofauti kabisa, Yanga ina wadhamini wengi ambao wanaweza ipa klabu pesa ya kuendeshea klabu lakini kubwa zaidio ni michango kutoka kwa Mashabiki yaani WANANCHI.
Timu kuendeshwa na wananchi maana yake unaruhusu Wananchi hawa kuwa na shinikizo la nguvu na haki kwa timu. Hii ina maana kuwa mashabiki wanaweza muondoa kocha.
YANGA YA MATOKEO.
Mashabiki wa Yanga wanachotaka ni matokeo tu na wala sio kitu kingine, haijalishi timu inachezaje lakini alama tatu ni muhimu kwa mashabiki wa Yanga kuliko kitu kingine.
Zahera naye ana nafasi kubwa ya kutokuwepo msimu ujao, kwanza ni Usajili wa Mwaka huu. Msimu uliopita Kila ya Yanga ilipofungwa, Zahera alisisitiza juu ya aina ya wachezaji waliopo kwa maana hawaendani na jinsi anavyotaka yeye.
Msimu huu Viongozi wamemuachia majukumu ya usajili. Ni kweli yeye aliacha majina yote ya wanaotakiwa kusajiliwa, na wote wamepatikana. Hii ina maana kuwa Timu imeshatimiza jukumu lake bado jukumu la kocha.
Jukumu la kocha katika hili ni kubeba ubingwa wa VPL na makombe mengine timu itakayoshiriki. Kushindwa kubeba kombe hali ya kuwa wachezaji wote aliowataka amewapata ni kutafuta kutimuliwa.
Njia pekeeya Zahera kuepuka hili ni kufanya vizuri katika mashindano ambayo hayakuwa katika mipango ya klabu yaani klabu bingwa Afrika.
Kwa Mfano Yanga ifike nusu au robo fainali klabu bingwa Afrika, hata isipobeba kombe la ligi lakini Zahera atakuwa na nafasi kubwa ya kubaki kuliko akishindwa kufanya yote.
HITIMISHO.
Katika kujenga msingi wa haya yote, kati ya Aussems na Zahera mmoja hatutakuwa naye msimu ujao, na huenda mwingine tukamuucha mapema kabla hata ya msimu kumalizika, inategemeana na matokeo katika ligi.
Jambo lingine la msingi ni kwamba, Simba na Yanga zote zina malengo yanayofanana. Kwa kuwa yanafanana basi mmoja lazima akose mwingine apate, kukosa kwake ndio kufukuzwa kwake.
Niambie
hapo chini, Unadhani ni nani ana nafasi kubwa ya kutimuliwa na huenda tusiwe
naye tena msimu ujao?