Sambaza....

Rais wa shirikisho la kandanda nchini (TFF) Wallace Karia amesema wataendelea kuisaidia timu ya Dar Young Africans katika ushiriki wao kwenye michuano ya Shirikisho Afrika.

Karia ameyasema hayo Jumamosi, May 19 wakati wa kulikabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara kwa timu ya Simba Sports Club.

Amesema wao kama taasisi wanakila sababu na wajibu wa kuisaidia Yanga kufanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwapa stahiki zote muhimu kwani wakifanya wao vizuri sifa zitarejea kwa TFF na nchi kwa ujumla wake.

Rais wa TFF, Karia

“Hatujaitelekeza Yanga, tunaisadia katika kila hali kwa namna ambavyo inaturuhusu, wakifanya wao vizuri na sisi kama Shirikisho ama nchi tunapata sifa, michezo yote ya nje tutatuma wawakilishi wetu ili waweze kuwa katika kila hatua,” Karia amesema.

Kwa sasa Yanga ambao wapo kundi D pamoja na timu za Gor Mahia, Rayon Sports na USM Alger wanashika nafasi ya mwisho wakiwa na alama moja pekee.

Yanga wamepata alama hiyo baada ya kutoka sare 0-0 na Rayon Sports katika mchezo wa pili wa kundi hilo, huku mchezo wa kwanza wakikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger.

Sambaza....