Sambaza....

Ukisikia jiji limewaka ! ndio hiki kinachotokea kwa sasa. Yote yanayotokea uwanjani ndio tafsiri halisi ya FOOTBALL, yaani mpira ni huzuni, mpira ni furaha, mpira ni hasira, mpira huogofya, mpira una raha zake.

Hatimaye Simba imefuzu hatua ya robo fainali katika kundi D ikiambatana na vinara Al- Ahly wenye alama 10, Simba 9, Vita na Saoura wakiwa na alama 8 na 7 mtawalia.

Magoli ya Mohamed Hussein Zimbwe na Clatus Chama yalitosha kuwalaza AS Club Vita kwa jumla ya goli 2-1, ushindi unahitimisha rekodi ya Simba kutofungwa uwanja wa taifa kwa mechi zote za nyumbani katika mashindano haya ya klabu bingwa Afrika.

Nimeufuatilia mchezo kwa umakini kiasi cha kumudu kuweza kuwapa alama wachezaji wa Simba kwa mujibu wa viwango vyao walivyovionyesha uwanjani. Alama hizi zitakuwa ni chini ya 10.

Mgawanyo wa alama hizi umezingatia majukumu aliyotimiza mchezaji akiwa na mpira na akiwa hana mpira, aina ya mikimbio yake, kuziba na kutengeneza nafasi kwa wengine.


Aishi Salum Manula. 8/10.
Alikaa golini akifanya kazi kubwa ya kulinda lango. Vita walipiga shuti 4 zilizolenga lango na Manula aliokoa 3, huku moja ikiwa ni goli. Manula ameonekana kuimarika zaidi katika eneo lake, hasa kudaka mipira bila kuachia.
Alikuwa mwepesi na mwenye haraka katika kuanzisha mashambulizi dhidi ya AS Club Vita. Kiufupi, Manula ametimiza majukumu yake vyema na anastahili kupata alama 8 kati ya 10.

Alitoka uwanjani akiwa na kadi ya njano, yenye madai ya kuchelewesha muda, lakini alifanya hayo yote ili tu kuisadia timu yake isonge mbele zaidi katika mashindano haya.


Mohammed Hussein, Zimbwe Jr. 8/10.
Beki kisiki wa kushoto. Namuita kisiki kutokana na kazi mujarabu aliyoifanya leo. Kwanza amefunga goli moja, ame-block mashambulizi mengi zaidi kuelekea langoni kwake.

Amepiga “successful tackle” moja, alitumika kama winga wa kushoto. Pale alipopata nafasi ya kushambulia, alifanya hivyo na alileta madhara, ndio maana ya goli lake. Anastahili kupata alama alizo zipata.

Paschal Wawa. 6/10
Miongoni mwa mabeki ngangari kwa sasa huwezi ukaacha kumtaja Sergie Paschal Wawa. Alituliza eneo la nyuma, kuipanga vizuri safu yake ya ulinzi, hasa kucheza vizuri “ recovery system” kwa mabeki wa kati na wa pembeni.
Alipiga mipira mirefu na mifupi kuwafikia viungo na kuanzisha mashambulizi kupitia kwa Zana Coulibaly na Mohammed Hussein. Hakuwa na utulivu kwa kiasi kikubwa, na hata goli lililofungwa na Vita lilikuwa na mchango wake.
Hakuwa mwepesi sana kuokoa mipira na kufanya “ marking” kwa wachezaji wa timu pinzani. Anastahili kupata alama 6 kati ya 10 na amevuka nusu.
Erasto Nyoni. 7/10.
Ametoka majeruhi lakini leo amekiwasha pale nyuma. Amekuwa msaada mkubwa sana kwa Paschal Wawa. Umbile na kimo chake kilimfanya ale sahani moja na washambuliaji wa Vita.

Mipira yote ya juu alikuwa akiiondosha kama ilivyo na mingi kuiokoa kwa kichwa. Hakuonekana sana akiwa na mpira kwa kuwa Simba leo, iliingia na “game plan” ya kushambulia muda wote, lakini yeye alikuwa akiziba nafasi za wapinzani kupiga mashuti langoni mwake.

Zana Coulibaly. 8/10.
Upande wake ulikuwa salama muda wote, alicheza juu na chini kwa wakati mmoja. Alipiga krosi, aliokoa mipira, alipandisha mashambulizi, alikuwa ni tishio kwa mabeki wa Vita.
Uwezo wake wa kupiga vyenga na kupiga krosi ziliifanya Simba kuendelea kuonyesha uhai na matumaini kwa mashabiki na kuwafanya wahanikize kwa nguvu zaidi.
Zana ameonyesha yeye ni beki wa aina gani. Aliokoa mipira ya mwisho akiwa yeye na lango lake, alikuwa mtulivu zaidi katika mechi hii, anastahili kupata 8 kati ya alama 10.
James Kotei. 6/10.
Mkata umeme huyu. Kotei hajawahi kumuacha mchezaji akatize na mpira pembeni yake bila kumfanyia chochote, amejithidi sana kwa ushirikiano na Mzamiru.
Lakini hata hivyo leo hakuwa katika kiwango kikubwa cha kumfanya asalie uwanjani kwa dakika tisini, alishindwa kuisaidia timu yake kupandisha mashambulizi. Anastahili kupata 6 kati ya 10.

Clatus Chama. 9/10
LUSAKA IGNEOUS ROCK, huyu ndiye hasa alikuwa na kiwango kikubwa. Leo alichezeshwa katika nafasi ya kiungo mshambuliaji na kuna wakati alicheza kama namba 10.
Nafasi kama hii alicheza dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatin na kuwalamba goli moja, nafasi sawa na aliyocheza dhidi ya Vita na kuwafunga pia.
Ubunifu kwake uliongezeka, alikaba na kupiga pasi za mwisho. Alikosa nafasi kadhaa za kufunga kwa kupiga mashuti lakini bahati mbaya mashuti yake yalikosa nguvu na shabaha.
Amefunga goli la ushindi katika dakika za magharibi ya Roho, sawa na alivyowafanya ndugu zake Nkana Red Devils ya nchini Zambia. Chama anastahili kupata alama 9 kati ya kumi, yaani leo alikuwa kileleni kimchezo.

Mzamiru Yassin 8/10.
Alichukua nafasi ya Jonas Mkude. Amefanya kazi kubwa na ya aina yake. Hakuruhusu kupitwa kirahisi rahisi. Mzamiru huwa ni mzuri akiwa hana mpira, yaani kukaba nafasi na watu, lakini katika mechi hii alikuwa vizuri kote.
Anastahili kupata alama 8 bila upendeleo. Yeye aliziba makosa ya Kotei na kumpa nafasi Clatus Chama kucheza kama kiungo mshambuliaji. Alikuwa mwepesi asiyekaa na mpira muda mrefu. Simba ilipoupoteza mpira aligeuka mbwa mwitu kuusaka mpira na kuurudisha katika umiliki.

John Bocco 5/10
Bocco hakuonekana sana akiwa na mipira lakini uwepo wake eneo la juu upande wa kushoto na kulia kuliifanya safu ya ulinzi ya Vita kujawa na uwoga.
Hakupata nafasi yoyote ya wazi, wala nafasi ya kutoa pasi ya mwisho lakini anastahili kupata nusu ya alama zote.

Meddie Kagere 6/10
Huyu hasa ndiye aliyekuwa akilindwa kwa macho zaidi ya mawili. Hadi mpira unaisha amekosa kutumia nafasi mbili za wazi. Uwepo wake uwanjani uliifanya beki ya Vita kushindwa kupanda na kufanya mashambulizi.
Vita ya Congo sio hii ya KWA MKAPA kwani mabeki wake licha ya kuwa warefu walishindwa kwenda kupiga vichwa kwa mipira ya kona kwa kumuhofia Kagere anaweza kuwadhuru. Anastahili kupata alama hizo.

Emmanuel Okwi 5/10
Ametoka kwenye majeruhi, lakini upambanaji wake ameuonyesha kwa dakika alizocheza, hakuwa na makli yaliyokuwa yanatazamiwa kutgoka kwake. Uwepo wake ndani ya dimba kuliwafanya mabeki wa pembeni kushindwa kunda na kumkaba kwa nguvu na umakini mkumbwa.
Kitendo hicho kiliwafanya washindwe kuwakaba wachezaji wengine wa Simba akiwemo Chama ambaye alionekana kucheza akiwa pekeyake. Anastahili kupata nusu ya alama zote.

Haruna Niyonzima 8/10
Utawataja wote lakini, Haruna ndiye mchezaji aliyeingia na kuchangamsha timu. Aussems alijua timu haikai na mipira, inakosa mbunifu wa kupiga pasi za mwisho, inakosa mtu wa kukaa na mpira japo kwa sekunde 5 hadi 10.
Haruna alifanya yote kwa wakati mmoja. Aliingia na kuongeza kasi ya mchezo. Aina ya mikimbio yake ndiyo iliyokuwa na faida sana kwa timu.
Amecheza dakika chache lakini anastahili kupata alama 8 kati ya 10, yeye alipiga kona na krosi hatari kuelekea langoni mwa Vita. Yeye alimpa nafasi nzuri Coulibaly kumimina krosi katika eneo hatari la Vita. Kiufupi Haruna alikuwa “ game changer” yeye ndiye hasa chachu ya ushindi wa Simba katika mechi hii.

Ushindi wa Simba unaifanya iungane na timu nyingine 8. Hatua ya makundi ilijumuisha jumla ya makundi manne, yaani kundi A, B, C, na D. katika kundi A, Wydad Casablanca na Mamelodi Sundowns zimeshafuzu, Kundi B,ni Esperance de Tunis na Horoya zimeshafuzu, Kundi C, TP Mazembe na CS Constantine zimeshafuzu pia na kundi D Al-Ahly na Simba zimeungana na nyingine kufuzu hatua ya robo fainali.

Sambaza....