Sambaza....

GOLIKIPA namba moja wa Yanga SC, Beno Kakolanya usiku wa Jumanne hii aliendeleza kiwango chake kizuri na kuisaidia timu yake kuendeleza vipigo kwa kila mpinzani wao anayekuja uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Beno ambaye ameruhusu goli moja tu katika michezo saba aliyocheza msimu huu aliiongoza Yanga kuichapa Lipuli FC bao 1-0 siku ya jana na kuwarudisha mabingwa hao wa kihistoria wa ligi kuu Bara katika nafasi ya pili ya msimamo.

Yanga ambao wamecheza michezo tisa msimu huu, wamefanikiwa kukusamnya alama zote 21 katika michezo yao ya nyumbani na nyingione nne katika michezo ya ugenini hivyo kufikisha alama 25- pointi mbili nyuma ya Azam FC wanaoongoza ligi wakiwa na alama 27 baada ya kucheza michezo 11.

“Sitazami rekodi zangu binafsi.” Anasema nyanda huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania nilipofanya mahojiano naye mafupi muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana. “ Tunatakiwa kuendelea kufanya kazi yetu kwa ufanisi zaidi kama tunahitaji kutwaa ubingwa. Ligi inazidi kuwa ngumu hivyo tunatakiwa kujituma zaidi katika kila mchezo ili kutimiza malengo yetu.”

Yanga ilisubiri hadi dakika za mwisho kiki ya faulo ya kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwapa alama tatu dhidi ya timu ya KMC FC inayocheza ligi kuu kwa mara ya kwanza wikendi iliyopita na walihitaji goli la juhudi binafsi kutoka kwa Mcongoman, Heritier Makambo kuifunga Lipuli FC Jumanne hii. Ushindi huo wa 1-0, 1-0 umewafanya baadhi ya mashabiki wao kutoamini kama wanaweza kufanya vizuri katika michezo ya nje ya Dar es Salaam.

“Waambie mashabiki wetu kuwa hii ni ligi na kila timu inaingia uwanjani kusaka ushindi. Kweli hatujashinda kwa idadi kubwa ya mabao katika michezo yetu miwili iliyopita lakini tumeshinda na kupata pointi sita. Hili ndiyo lengo letu. Tunakiwa kushinda kila mchezo bila kujali idadi ya magoli lakini tutafanyia kazi mapungufu yetu tupate ushindi mkubwa zaidi lakini muhimu ni kupata kwanza alama tatu.” Anamaliza kusema Beno.

Sambaza....