Wakati jana timu ya Simba SC imeanza kufanya mazoezi mepesi katika uwanja wao wa mazoezi wa Mo-Simba Arena uliopo Bunju , Dar es Salaam , baadhi ya wachezaji wa Simba SC bado hawajafika mpaka sasa hivi ni wachezaji watatu ambao ni Shiboub , Chama na Kahata.
Mtandao huu ulienda kushuhudia mazoezi ya Simba moja kwa moja kwenye dimba lao la Mo-Simba Arena na tukapata nafasi ya kuzungumza na meneja wa Simba SC , Patrick Rweyemamu. Ambapo alitubainisha kuwa wachezaji wamefanyiwa vipimo.
“Mpaka sasa hivi wachezaji 26 wamefanikiwa kufika kwenye mazoezi na wachezaji watatu pekee ndiyo hawajafanikiwa kufika kwenye mazoezi na hawa wachezaji 26 waliofanikiwa kufika kwenye mazoezi wamefanyiwa vipimo na daktari wa timu ndiye atatoa majibu ya vipimo husika”- alisema meneja huyo wa Simba SC
Kuhusu wachezaji ambao hawajafika aliwataja ni Chama , Kahata na Shiboub ambapo amedai kuwa kwa sasa wanafanya kila wawezalo ili kuhakikisha wachezaji hao wanarudi na kuungana na wenzao.
“Mpaka sasa hivi ni wachezaji watatu tu ambao hawajafika kwenye mazoezi , Kahata ambaye nchi yake ina lockdown ya mkoa kwa mkoa kitu ambacho ni ngumu kwake yeye kutoka na tunajitahidi kuona namna gani ambavyo anaweza kusafiri na kuja , Shiboub naye nchi yake ina lockdown lakini Chama muda wowote anaweza akafika nchini”-alimalizia meneja huyo