Tanzania ishawahi kuwa na Kipre , huyu unaweza kumsimulia kwa hadithi tofauti kabisa. Mu-Ivory Coast aliyekuja Tanzanià kutengeneza barabara la kupitishia gari la chakula kwenda tumboni.
Huyu alikuja kufanya kazi kweli na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Alikuwa mhimili mkubwa sana pale Azam Fc.
Wakati Azam FC wakiwa na bahati ya kuishi na Kipre, Simba nao waliwahi kupata bahati kubwa ya kuwa na Mavugo.
Hii ilikuwa bahati kubwa sana kwa sababu Mavugo wakati anakuja Simba, alikuja kama mfungaji bora wa ligi ya Burundi.
Kwa hiyo Simba ilikuwa imepata mfungaji ambaye alikuwa anatazamiwa kuwa na msaada mkubwa .
Lakini wote hawa wawili mwisho wao ulikuwa tofauti kabisa kama ambavyo ulivyokuwa mwanzo wao.
Mwanzo wa Kipre ulikuwa tofauti kabisa na mwanzo wa Mavugo.Kipre alikuja Azam Fc kama mchezaji kijana.
Mchezaji ambaye alikuwa bado hajakomaa kuwa mchezaji mkubwa. Kwa kifupi kumchukua Kipre ilikuwa ni kwa asilimia kubwa ni kamari.
Sawa alikuwa na kipaji, lakini alikuwa kijana ambaye ndiye anakuwa, kijana ambaye bado alikuwa hajadhitisha kupitia kipaji chake.
Kwa hiyo alikuja kudhitisha kipaji chake na kupevuka vizuri akiwa katika jezi ya Azam Fc. Na ndipo hapo watu wengi wakamjua.
Hii ilikuwa tofauti kabisa na kwa upande wa Mavugo. Vitabu vya hadithi ya mpira wa miguu vinanionesha kuwa Mavugo amekuja Simba kama mchezaji ambaye tayari ameshapevuka.
Amekuja Tanzania akiwa tayari ameshakuwa mfungaji bora katika ligi ya Burundi.
Simba walikuwa wamempata mchezaji ambaye tayari alikuwa ameshapevuka vizuri kwa ajili ya kuisaidia Simba.
Hii ndiyo ilikuwa tofauti kubwa sana kati ya Mavugo na Kipre, utofauti huu unaweza kuuweka kwenye sentensi moja ambayo itakufanya uelekewe vizuri.
Mavugo alikuja Simba kama shujaa, na Kipre alikuja Azam Fc kama mtu ambaye anatakiwa kuutengeneza ushujaa wake.
Kipre alifanikiwa sana, alitengeneza ushujaa wake vizuri na mwisho wake pale Azam Fc ulikuwa bora zaidi kuliko mwisho wa Mavugo.
Pamoja na kwamba Mavugo alikuja kama shujaa pale Simba, lakini aliondoka akiwa hana hilo vazi la ushujaa.
Vazi ambalo Kipre aliondoka akiwa amelivaa vizuri na ndiyo maana hata pengo lake imekuwa ngumu sana kwa Azam Fc kuziba pengo lake.
Tangu Kipre aondoke Azam Fc imekuwa ngumu kumpata mtu sahihi ambaye anaweza kuivaa nafasi yake kwa kiasi kikubwa.
Leo hii Azam FC ina Obrey Chirwa , mtu ambaye anacheza katika eneo ambalo Kipre alikuwa anacheza kipindi chake.
Kitu hiki huwa kinanifanya nimkumbuke sana Kipre, kwa sababu viatu vya Kipre vimempwaya sana Obrey Chirwa.
Obrey Chirwa anaweza akawa na nguvu kubwa sana, akawa na uwezo mkubwa wa kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
Lakini mwisho wa siku ambacho huwa anakosa ni namna ambavyo anaweza kumalizia mpira wa mwisho.
Maamuzi yake ya mwisho baada ya kufanya kazi kubwa ndiyo yanayomtofautisha Kipre na Obrey Chirwa.
Kipre alikuwa anafanya kazi kubwa sana akiwa anapambana na mabeki, na maamuzi yake ya mwisho yalikuwa bora.
Yani mpira wake wa mwisho ulikuwa bora sana. Alikuwa na uwezo wa kutoa pasi nzuri ambayo inaweza kuwa na faida kubwa kwa timu.
Pia alikuwa na uwezo wa kufunga. Hii ni tofauti sana na Obrey Chirwa. Huwa anatumia nguvu nyingi sana.
Lakini maamuzi yake ya mwisho, yani mpira wake wa mwisho huwa unakuwa tofauti kabisa.
Anaweza akatoa pasi ya mwisho ambayo unaweza ukatoa chozi. Anaweza kukosa nafasi nyingi za wazi ambazo unaweza ukauzunika.
Huyu ndiye anayefanya hadithi ya Kipre ikumbukwe sana. Hii ni tofauti kabisa na kwa Simba na hadithi yao ya Mavugo.
Mavugo alikuja Simba kama mtu ambaye anatazamiwa kufanya mazuri sana kutokana na kiwango chake.
Lakini mwisho wa siku hakuna alichokifanya baada ya hapo. Nani alifuata?, bila shaka ni Meddie Kagere.
Meddie Kagere amekuja kutufanya tusikumbuke kama kuliwahi kutokea mtu ambaye anaitwa Mavugo.
Anafanya makubwa zaidi ambayo Mavugo aliwahi kuvifanya. Meddie Kagere mpira wake wa mwisho una madhara makubwa sana kuliko mpira wa mwisho wa Mavugo.
Ndiyo maana ana wastani mzuri wa kufunga na kutoa pasi za mwisho kuliko Mavugo ambaye alikuja na ushujaa kwenye mbuga ya msimbazi, mbuga yenye Simba na akasahau yeye ni chakula cha Simba.