Sambaza....

Uongozi wa klabu ya soka ya Kagera Sugar ‘Wanankurukumbi’ umesema umeridhika na mwenendo wa ligi ikiwa tayari imekwisha kucheza michezo miwili mpaka hivi sasa na kukusanya alama nne.

Katibu mkuu wa Klabu hiyo Hussein Madaki amesema matokeo ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mmoja siyo mabaya sana na kocha Mecky Mexime atajaribu kuangalia makosa yaliyojitokeza ili waweze kufanya vizuri katika mchezo ujao dhidi ya Biashara United.

“Naona sio mbaya sana kwa sababu tumeshacheza mechi mbili, tumeshinda moja tumetoka sare moja, mwalimu bado ana kazi ya kufanya ili kuhakikisha tunapoanza kutoka ugenini tunakwenda kutafuta pointi nyingine zaidi ili kujijengea mazingira mazuri mapema,” Madaki amesema.

Baada ya mapumziko ya kupisha majukumu ya timu ya Taifa, Kagera Sugar watasafiri hadi mkoani Mara kucheza na Biashara United, na Madaki amesema wamewapa wachezaji mapumziko ya siku mbili kabla ya kurejea tena katika maandalizi ya mchezo huo.

“Wachezaji wamepewa mapumziko ya siku mbili na Jumanne watarejea tena na kuanza na mazoezi kama kawaida, timu itaendelea kuwa kambini hadi kwenye mchezo huo wa Musoma na baada ya hapo tutaelekea Mkoani Mbeya,” amesema.

Kagera Sugar walianza ligi kwa kucheza na Mwadui FC na kuwafunga mabao 2-1 kabla ya kucheza na African Lyon na kutoka suluhu, michezo yote miwili ilipigwa katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Sambaza....