Sambaza....

Mara ya mwisho kwa Yanga kupata cleansheet ilikuwa lini?, wakati unajiuliza jibu sahihi la swali hili kuna kitu pia unatakiwa kujiuliza sana.

Kwanini Yanga ilikuwa inapata Cleansheet nyingi kipindi cha Beno Kakolanya tena akiwa na mabeki wale wale ambao wako na Ramadhani Kabwili?

Mabeki ambao hawampi Cleansheet tena Ramadhani Kabwili kama ambavyo walivyokuwa wanampa Beno Kakolanya ?

Kuna kitu kimoja ambacho unatakiwa kukifanya vyema, upatikanaji wa Cleansheet unategemeana na uimara wa safu ya ulinzi.

Safu ya ulinzi hujumuisha kipa pamoja na idara ya ulinzi. Hawa wakiwa imara lazima kabisa timu Iwe na uhakika wa kupata Cleansheet (s) nyingi.

Sasa basi kuna kitu kimoja hapa cha kuangalia kwa undani, unapokuwa na mabeki imara unatakiwa uwe pia na kipa imara.

Kipa imara haiishii kuwa imara kwa kutoa michomo mikali tu ndani ya mchezo , La Hasha! , kipa imara lazima awe pia kiongozi imara.

Uongozi ndiyo unaoifanya safu ya ulinzi Iwe imara pia kwa sababu kiongozi huwaongoza wao kusimama vizuri.

Sasa kuna kitu kimoja ambacho kwa Ramadhani Kabwili hana, na hiki kinaweza kupatikana kwa yeye kujifunza kwa mtu ambaye anaonekana ni bora.

Ramadhani Kabwili hujisahau kwenye mengi sana anapokuwa langoni mwake. Moja, huwa anajisahau sana anapokuwa anatakiwa kuwapanga mabeki wake.

Na kuwakumbusha majukumu yao kipindi ambapo wanapojisahau kutimiza majukumu yao kwa wakati husika ndani ya mchezo.

Kwenye mechi dhidi ya Simba kuna baadhi ya mabeki walikuwa wanahasau majukumu yao ya kimsingi ndani ya uwanja.

Mfano, Gadiel Michael alikuwa anapanda sana na kusahau kurudi kwa wakati nyuma kwa ajili ya kuzuia kipindi timu inapokuwa haina mpira.

Kitu hiki kilikuwa kinasababisha Yanga kuwa na uwazi sana eneo la nyuma kwa upande wa kushoto, uwazi ambao aliutumia John Bocco kupita krosi ambayo ilisababisha goli.

Beno

Hapa kuna kipi cha kujifunza ambacho Ramadhani Kabwili anatakiwa kujifunza?, Ramadhani Kabwili ndiye msaidizi mkubwa wa Mwinyi Zahera kwenye idara ya kiungo.

Yeye ndiye anayeiona timu vizuri kwa sababu iko mbele yake, yeye ndiye anayeona ni nani hayuko katika eneo sahihi na ni jukumu lake kumkumbusha.

Haiitaji Mwinyi Zahera kumbusha mchezaji husika wakati Ramadhani Kabwili yupo kwa ajili ya kumsaidia kocha wake kuwakumbusha mabeki kipindi wanapojisahau kutimiza majukumu yake ya msingi.

Pili, ukitazama goli la Mbao, pamoja na kwamba alifanya maamuzi ambayo siyo sahihi kuufuata ule mpira ambao alikuwa hana uwezo wa kuufikia.

Pia Ramadhani Kabwili alikuwa hajawapanga vizuri mabeki wake kuuzuia mpira ule wa krosi. Na mipira mingi ya krosi alikuwa hawapangi vizuri mabeki wake.

Ramadhani Kabwili anakosa hali ya kuwa kiongozi ndani ya timu. Hali ambayo alikuwa na nafasi nayo kubwa sana kujifunza kutoka kwa Beno Kakolanya.

Beno Kakolanya ambaye amekomaa vizuri kuwa kipa imara, kipa mwenye uzoefu mkubwa kwenye mpira wetu wa Tanzania.

Lakini muda huu Ramadhani Kabwili yupo katika muda ambao hana sehemu nzuri ya yeye kujifunza. Hana sehemu nzuri ya kumjenga kuwa kipa imara.

Umri wake ni mdogo sana , alitakiwa kuwa chini ya mtu ili tu aweze kukuzwa katika mazingira ambayo yangemfanya yeye awe bora zaidi.

Sambaza....