Baada ya kufika salama Sumbawanga mkoani Rukwa watoza ushuru wa Kinondoni KMC watakuwa dimbani kesho kuvaana na Tanzania Prisons katika dimba la Nelson Mandela mkoani humo.
Akiongea na tovuti ya Kandanda.co.tz Christina Mwagala msemaji wa KMC, ameelezea kuhusu hali ya kikosi na maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons hiyo kesho “Kesho kikosi cha timu kubwa Barani Afrika KMC Fc wana “Kino Boys” tutakua tena ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi ya NBC Tanzania Bara mechi ambayo tutacheza saa 10 kamili jioni.”
Ikiwa ni mchezo wake wa tatu toka apewe timu Kocha wa kikosi hicho cha KMC Jamhuri Kiwelu Julio ameeleza kuhusu hali ya wachezaji wake, hali ya hewa (baridi) na maandalizi ya kuwakabili Tanzania Prisons kesho “Hali ya hewa ni ngumu lakini sisi tumeizoea kwasababu kabla ya kuja huku tulikwenda Makambako tukaweka kambo kule lakini kwa bahati mbaya tukaambiwa mechi zimesogezwa mbele, tukarudi Dar kwa siku chache lakini tukarudi tena Sumbawanga tarehe 1 kwahiyo maandalizi yetu yako vizuri na wachezaji wako vizuri.”
Akielezea kuhusu mchezo wa kesho Julio alisema “mchezo utakua mgumu na tunawaheshimu Prrisons kwani wao sio timu ya kitoto, ni timu ambayo ina uwezo wake, ni timu ambayo ina wachezaji wazuri lakini vilevile hata sisi timu yetu ni nzuri na ni bora vilevile, tutapambana kesho kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu ili zituweke vizuri ili tusishuke daraja na kuikimbia “Playoff” naamini tutafanikiwa kwasabu vijana wangu wako bora”.
Hakuishia hapo Julio aliiambia Kandanda.co.tz juu ugumu na ubora wa mpinzani wanaekwenda kupambana nae na namna watakavyomkabili.
“Nawaheshimu Prisons lakini sina hofu kwasabu timu ni zile zile ambazo tunazifahamu, na mimi nazifahamu vizuri timu za Tanzania na niseme tuu nimeiandaa vizuri timu yangu kwaajili ya kushinda mchezo wa kesho naamini tutashinda” alisema Julio.
Kuelekea mchezo wa kesho KMC itawakosa baadhi ya nyota wake kadhaa kutokana na majeraha. Kocha Julio hakusita kulizungumzia hilo lakini alitoa rai na wito kwa mashabiki na wanaipenda KMC kuendelea kuwatia nguvu na kuwaombea.
“Tutamkosa Ibrahim Ame na Matheo Antony, lakini sio tija sababu tulisajili wachezaji 26, niseme tuu wachezaji wangu waliosalia wako vizuri na tutafanya vizuri. Ninachowaomba wanaoipenda KMC watuombee kwa Mwenyezi Mungu ili wachezaji wawe salama mpira watuachie sisi” kocha Julio alimaliza.
Mchezo wa kesho utakua mgumu sana kwa KMC kulingana na mpinzani anayekwenda kukutana naye kwani Tanzania Prisons ni timu inayosifika kwa matumizi makubwa sana ya nguvu. Yote kwa yote utakuwa mzuri na wakuvutia zaidi.