Jkt Tanzania mabingwa wa zamani wa Kombe la FA walioshuka daraja misimu miwili iliyopita ni wazi sasa wanakaribia kurejea Ligi Kuu baada ya kubakisha ushindi katika michezo miwili pekee.
Mpaka sasa JKT imeshuka dimbani mara 24 wakiwa kileleni mwa Ligi ya Champioship kwa alama zao 59 walizokusanya mpaka sasa wakifuatiwa na Kitayosce wenye alama 50 na Pamba katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 48.
JKT wanahitaji kupata alama sita pekee katika michezo yao mitano iliyobaki ili waweze kujihakikishia kupanda na kurejea katika Ligi Kuu, maafande hao wanatumia uwanja wao wa nyumbani Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni JKT nje kidogo ya Jiji.
Mpaka sasa JKT ndio timu pekee iliyofunga mabao mengi [mabao 41] na kuruhusu machache zaidi [mabao 12] na kuifanya kuwa timu pekee katika Ligi ya Championship yenye wastani mzuri magoli ya kufunga na kufungwa.
Wanajeshi hao wamedhamiria kupanda Ligi na si ajabu kufanya kwap vyema kunatokana na kusheheni mastaa kibao waliowahi kutesa na timu za Ligi Kuu. Baadhi ya nyota wa JKT Tanzania ni pamoja na Hassan Kapalata [Zamani KMC na TZ Prisons], Edward Maka [Zamani Yanga], Ally Makarani [Mtibwa Sugar], Omary Ramadhani “Berbatov” [Zamani Ndanda na KMC] na Edward Songo nahodha.
Nyota wote hao wapo chini ya mwalimu mwenye uzoefu na soka la Tanzania, kocha wa zamani wa Ndanda na Polisi Tanzania Malale Hamsini Malale.