Simba kwa mara ya tatu mfululizo anashindwa kupata matokeo katika michezo yake ya michuano tofauti anayoshiriki msimu huu. Wanafungwa mara mbili katika klabu bingwa Afrika halafu wanatoka sare katika Ligi Kuu ya NBC.
Jumamosi Simba walikufa mabao matatu kwa bila dhidi ya Raja Casablanca sehemu ambayo inajulikana si salama kwa wageni katika michuano ya kimataifa, halafu wanapata sare na Azam ya bao moja kwa moja siku nne mbele katika mchezo wa Ligi Kuu.
Katika michezo yote miwili unaona ni dhahiri shahiri Simba walistahili walichokipata. Ngome ya Simba inafikika kirahisi mno na wapinzani iko “very exposed”. Rejea mchezo dhidi ya Mbeya City halafu wa Raja na huu waliotoka sare dhidi ya Azam Fc. Pengine hata mchezo waliopata mabao mengi dhidi ya Prisons huenda ungekua mgumu kwao kama kusingekua na kadi nyekundu kwa wapinzani.
Siku ya kwanza Robertinho akiwa kazini katika mchezo dhidi ya Mbeya City alilazimika kumtoa Chama dakika ya 33 ya mchezo na kumuingiza Pape Sakho baada yakuona mbinu zake haziendi kama ambavyo anataka uwanjani. Si mashabiki waliojitokeza uwanjani tuu hata waliokua nyumbani hawakukubaliana nae.
Tangu hapo Robertinho amekua akilazimisha kuwachezesha Saidoo na Chama wote kwa pamoja na matokeo yake ndio haya tunayoyaona. Kiuhalisia Chama na Saidoo ni wachezaji wa aina moja (namba 10). Ni wazuri na “productive” zaidi wakicheza nyuma ya mshambuliaji.
Na haikua ajabu Simba walimsajili Saidoo kutoka Geita ili kwenda kumsaidia Chama kuongeza ubunifu baada yakuona ni kwa jinsi gani timu ilikua inashindwa kutengeneza nafasi pindi Chama akiwa hayupo kiwanjani. Na ulikua usajili sahihi kabisa wa dirisho dogo kwa Simba.
Jinsi Chama na Saidoo wanavyoikaba Simba
Sababu ya kwanza!
Sasa makocha wa Simba wanalazimika kuwapanga Chama na Saidoo kwapamoja ambao ni wazuri timu ikiwa na mpira lakini baada yakupoteza mpira wanakua na mchango hafifu katika ukabaji. Na hii inakuaga mara nyingi ni asili ya wachezaji wa aina yao “mafundi” wanapenda zaidi kuchezea mpira na sio kuukimbiza mpira, lakini pia hata umri unawatupa mkono wanakosa ile nguvu yakureact kwa haraka pindi wanapotakiwa kukaba. Hii maana yake inawaacha Simba ikiwa na watu watatu mpaka wanne ambao hawakabi timu ikiwa inashambuliwa. ( Chama, Saidoo na Baleke/Bocco na pia wakati mwingine Sakho).
Sababu ya pili!
Pia kwakumpanga Saidoo namba 10 halafu Chama winga moja na winga nyingine huanza Sakho, ambapo mara nyingi Chama huingia ndani na kumfanya Shomary Kapombe au Mohamed Hussein kupanda na kushambulia kwakutokea pembeni na hapa ndio tatizo lapili huonekana. Na mara nyingi Kapombe huwa ndio muhanga wa hili, hujikuta amekwenda kushambulia kwa kupiga kross ama kukata ndani ya boksi na kuacha eneo lake likiwa wazi hivyo kuwapa wapinzani nafasi kubwa yakushambulia nafasi anayoiacha ambapo humfanya mlinzi mmoja wa kati kwenda kuziba eneo lake (Rejea bao latatu walilopata Raja kwa mkwaju wa penati).
Sababu ya tatu!
Kumpanga Chama na Saido pia kunaifanya Simba kushambulia kwa idadi kubwa lakini pasi na kutimia ndani ya box la wapinzani maana wote hawa sio wazuri sana katika mipira yakugombania na hivyo mara nyingi wakishindwa kushambulia kwa pasi mpaka ndani ya box la mpinzani basi watamuacha mshambuliaji apambane mwenyewe katika mipira ya kross na hivyo inakua rahisi walinzia wa timu pinzani kushinda mipira yote. (Rejea mchezo dhidi ya Raja)
Hitimisho!
Ni vyema sasa walimu wa Simba Mgunda na Robertinho wakakubali yaishe na kumuanzisha mmojawapo kati yao haswa pindi Simba inapocheza na wapinzani “heavy weight” aina ya Raja Casablanca, Azam na hata Yanga katika uwanja mzuri kama wa Benjamin Mkapa.