Sambaza....

Jana zilipatikana dakika 72 za kwanza za Alexis Sanchez.

Dakika 72 ambazo zilimwezesha awe mchezaji bora wa mechi ya jana ya FA CUP dhidi ya Yeovil Town.

Hii inatoa tafasri moja, ulikuwa mwanzo mzuri wa Sanchez ikizingatia kila jicho lilikuwa linamtazama yeye kila aliposhika mpira.

Lakini hofu aliishusha chini, akawa hana presha kubwa juu ya mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Manchester United.

Miaka 3 amekuwa nchini England, akicheza Arsenal. Hakuwa mgeni na soka la Englnad hali ambayo ilimfanya yeye asiwe na wakati mgumu katika mchezo wake wa kwanza.

Jana Manchester United walicheza mfumo gani ?

Kwenye karatasi Manchester United walianza na mfumo wa 4-3-3, lakini kwenye uwanja ilikuwa tofauti, kwani walikuwa wanacheza mfumo wa 4-3-2-1. Mabeki wa kati wakiwa Rojo, Lindelof. Beki wa pembeni kulia alikuw a Darmian na beki wa pembeni kushoto alikuwa Luke Shaw.

Wakati viungo watatu wa kati walikuwa Carrick, Scott McTommy na Ander Herrera.

Mbele yao alicheza Mata ambapo eneo la kushoto mbele alicheza Sanchez ambaye alikuwa anatokea pembeni kushoto akiingia katikati , huku Rashford akiwa mchezaji wa mwisho.

Yeovil Town walicheza mfumo wa 4-4-2 , ambapo uliwawezesha kipindi cha kwanza wacheze kwa kuelewana na kujilinda vizuri.

Njia pekee ambayo walikuwa wanaitumia kujilinda ni kuhakikisha hawatengenezi uwazi eneo la nyuma ndiyo maana kipindi cha kwanza ilikuwa ngumu kwa Manchester United kutengeneza nafasi nyingi za wazi kwa sababu hakukuwepo na uwazi sehemu ya nyuma ya Yeovil Town.

Pia wachezaji wa Yeovil Town walikuwa wana “mark” kila mchezaji wa Manchester United alipokuwa anapata mpira.

Hivo wachezaji wa Manchester United hawakuwa huru kutengeneza nafasi kila wanapopata mpira kwa sababu wachezaji wa Yeovil Town waliwakaba “man to man”.

Yeovil Town walikuwa wanashambulia kwa kutumia mipira ya moja kwa moja “direct football” ingawa hawakuweza kutumia vizuri mashambulizi yao kwa sababu ya kukosa ukomavu.

Kuna wakati Yeovil Town waliwalazimisha Manchester United kufanya madhambi karibu na eneo lao , kwa kipindi cha kwanza pekee Manchester United walifanya madhambi mara 7 dhidi ya mara 3 ya Yeovil Town, lakini Yeovil Town hawakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi mazuri ya mipira ya adhabu waliyokuwa wanaipiga.

Manchester United walibadilisha mfumo kipindi cha pili.

Baada ya Lukaku kuingia nafasi ya Mata, Manchester United walicheza 4-3-3 halisi ambapo katikati walibaki Carrick, Scott na Herrera na mbele wakabaki Sanchez kushoto, Rashford kulia na katikati akasimama Lukaku.

Kipindi hiki cha pili Yeovil Town waliachia uwazi katika maeneo mengi ya uwanja hasa hasa nyuma ndipo hapo Manchester United walitumia vizuri nafasi hiyo ambapo kipindi cha kwanza hakukuwepo na uwazi katika maeneo ya nyuma ya Yeovil Town.

Baada ya Sanchez kuondoka na kuingia Lingard Manchester United walirudi tena kwenye mfumo wa 4-3-2-1, ambapo Lingard alikuwa anatokea katikati na kucheza nyuma ya Lukaku aliyesimama kama mshambuliaji wa mwisho wakati Rashford akicheza pembeni kushoto.

Je Luke Shaw anatakiwa kuongezewa mkataba ?

Amekaaa muda mwingi akiwa majeruhi, ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi cha Manchester United ambaye ni namba tatu halisi.

Mkataba wake unaisha katika majira ya joto, lakini kadri muda unavyozidi kwenda anaonesha kuwa anastahili mkataba mpya kulingana na kiwango chake anachokionesha baada ya kuaminiwa.

Sanchez atarudisha heshima ya jezi namba saba?

Bryan Robson ambaye alikuwa anajulikana kama “Captain Marvel”) alikuwa na kiwango kizuri na kikubwa chenye mafanikio makubwa akiwa na jezi namba 7, ambapo baadaye Eric Cantona alifanikiwa kupata mafanikio makubwa na jezi hiyo kama ilivyokuwa kwa David Beckham na Cristiano Ronaldo.

Baada ya Cristiano Ronaldo kuihama timu hii mwaka 2009 hakuna mtu aliyefanya vizuri na jezi hii.

Walivaa kina Michel Owen, Di Maria, Valencia , Depay lakini hakuna aliyefanya vizuri na jezi hii. Valencia alivaa mwaka mmoja akairudisha.

Ni jezi nzito katika klabu ya Manchester United, leo hii Sanchez amepewa aibebe mgongoni, mafanikio aliyoyapata na Arsenal , kwa kiwango kile alichokionesha katika nchi ya England kwa miaka 3 kunampa nafasi ya kufanya vizuri na jezi hii ingawa umri unamnyima nafasi ya kufanya makubwa zaidi

Sambaza....