Sambaza....

Hapana shaka ndiye mchezaji bora wa Simba na wa ligi kuu msimu huu, hili ndilo neno pekee ambalo ninaweza kuanza nalo ninapoandika makala hii.

Shiza Ramadhani Kichuya alisifiwa sana wakati anakuja msimbazi na mimi sikutaka kumsifia nilimpa tafadhari moja tu kwenye andiko langu “Kichuya karibu kwenye kioo cha kinyozi”.

Kioo hiki hubeba taswira za kila sura, kila aina ya nywele huonekana kwenye kioo hiki cha kinyozi, kinyozi hujitahidi kukunyoa kwa ustadi mkubwa kipindi mifuko yako inapokuwa minene, wembamba wa mifuko unapokaribia hata kipande cha chupa huwa kifaa kizuri kwa ajili ya kukunyoa.

Hakuna jema linalokumbukwa kwa wepesi kipindi unapokuwa umeshuka, kelele zile zilizotumika kukushangilia kipindi hiki zinaweza kutumika kukuzomea. Hakuna atakayekumbuka kona uliyoipiga kwenye mechi dhidi ya Yanga.

Kipindi hicho hisia za hasira na chuki zitakuwa zimekaa karibu yao. Kichuya alinisoma na kunielewa vizuri sana hasa hasa mstari niliomwambia afungue macho na atazame mbali.

Mbali ambako kuna faida kubwa kwake kuliko hapa alipo, miaka kadhaa imepita yuko ndani ya kikosi cha Simba, kikosi ambacho kwa sasa kimebeba ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara msimu huu.

Kuna mengi sana ya kuyatazama kwa jicho la hongera kuhusu safari ya Simba msimu huu, hapana shaka viongozi wanahitaji hongera, benchi la ufundi na wachezaji wanastahili pongezi za dhati.

Lakini kuna kitu kimoja hubaki na lazima kibaki kiwe kimesimama peke yake kwa sababu hakuna usawa kabisa kwenye dunia hii isiyokuwa sawa.

Huwezi kupata usawa kwenye sayari hii ndiyo maana Manchester City msimu huu pamoja na timu kuonekana inacheza vizuri kwa pamoja lakini Kelvin De Bryune anabaki kama mchezaji bora katika kikosi hicho msimu huu.

Hapana shaka yeye ndiye alikuwa mkandarasi bora wa uimara wa Manchester City msimu huu mpaka wakachukua ubingwa.

Uimara wake ulikuwa nguzo mahiri katika kikosi cha Manchester City sema hakuwa mfungaji mzuri kama Sergio Kun Aguero au Mohamed Salah ndiyo maana tunaweza tukapunguza utamu wa mashairi yetu kwake.

Ndivyo ilivyo kwa Simba, tunaweza tusitumie muda mwingi kumpa nafasi Shaban Robert kuandika shairi la jina la Kichuya na tukampelekea majina mawili tu Emmanuel Okwi na John Bocco.

Hii ni ƙkwa sababu Shiza Kichuya hajafunga sana kama alivyofunga Emmanuel Okwi na John Bocco.

Lakini pamoja na kutofunga magoli mengi lakini ndiye anabaki kuwa mpaka rangi bora katika jumba la ubingwa wa msimbazi msimu huu.

Amekuwa akicheza nafasi ambayo anakuwa huru kiwanjani. Kuna muda utamuona pembeni kushoto, pembeni kulia, nyuma ya kina Emmanuel Okwi na John Bocco pia unaweza kumuona katikati ya uwanja.

Hii inamsaidia kitu kimoja, kuwa mtu ambaye anatengeneza mashambulizi ya Simba ( building up ya mashambulizi ya Simba yanaanzia kwake).

Yeye ndiye mchonga barabara ya mashambuliaji ya Simba, unapoona Simba imefunga magoli mengi msimu huu mtu pekee aliyekuwa anasuka mipango ya magoli kwa wingi ni Shiza Ramadhani Kichuya.

Magoli 34 ya Emmanuel Okwi na John Bocco kwa pamoja mengi yametokana na sababu hizi mbili. Mosi yeye ndiye alipiga pasi za mwisho, pili yeye ndiye aliyetengeneza nafasi ndani ya uwanja.

Amehusika kwenye magoli mengi kuzidi mchezaji yoyote ndani ya ligi kuu msimu huu, hakika alikuwa Afisa mipango wa ubingwa msimu huu.

Tunaweza kuwasifu sana kina Emmanuel Okwi, tukawashangilia sana kina John Bocco lakini shujaa wa Simba msimu huu atabaki kuwa Shiza Ramadhani Kichuya.

Huyu ndiye mchezaji bora wa Simba na ni mchezaji bora wa libi kuu msimu huu lakini hatuwezi kulitazama hili kwa kina kwa sababu Shiza Ramadhani Kichuya hafungi sana kama ilivyo kwa Kelvin De Bryune.

Sambaza....