Siyo jambo la busara na siyo la kibusara kabisa kwa shabiki wa mpira wa miguu kufanya shambulio kwa mtu kutokana na aina ya matokeo yanayopatikana ndani ya uwanja. Huu ni ukosefu wa nidhamu, nidhamu ambayo huwa tunaihubiri kila Siku kwa wachezaji wetu kuwa nayo, na kwetu sisi mashabiki tunatakiwa kuwa nayo.
Tuivae nayo, tutembee nayo huku tukijua mpira ni mchezo unaoleta burudani kwa mashabiki wa mpira wa miguu. Kuna aina mbili ya mashabiki, mashabiki wa timu A na mashabiki wa timu B. Burudani isipopatikana kwa shabiki wa timu A bali shabiki wa timu B atapata burudani, na kumwacha shabiki wa timu A akiwa na majonzi. Hizi ndizo hisia mbili ambazo zinazalishwa kwenye mpira wa miguu.
Hisia ya furaha na hisia ya majonzi. Lazima kila shabiki azipitie hizi hisia. Hakuna mwenye hatimiliki hata mmoja wa kupata furaha peke yake tena kila siku kwenye mpira na huku mwenzake apate huzuni tu kila siku. Hakuna timu ambayo imeandikiwa ushindi kila siku!, hakuna timu ambayo imeandikiwa kila siku ishinde kwa idadi kubwa ya magoli, Haipo! na kama ipo basi mwenyezi MUNGU yupo kwenye uumbaji wa timu hiyo.
Ila kwa sasa hajafanikiwa kuumba timu yenye kushinda kila mechi tena kwa idadi kubwa ya magoli tena kwenye dunia hii ya ushindani. Kujipa hatimiliki ya ushindi kwenye kila mechi kunatoa maana halisi ya neno “ushindani”. Kuna haja gani ya kuanzisha ligi ili timu zishindane ilihali kuna timu ambayo imejipa hatimiliki ya kushinda kila mechi?
Hakuna haja, ndiyo maana mimi binafsi huwa naielewa sana ile kauli ya kuwa ” usiende na matokeo ndani ya uwanja”. Tunatakiwa kwenda uwanjani kwa kuamini kuwa kila timu ina nafasi ya kushinda hata kama ni finyu. Tunatakiwa kwenda uwanjani huku tukijua kuwa michezo ni sehemu ambayo inaleta umoja na mshikamano hivo ni lazima tudumishe amani kwenye viwanja vyetu.
Tumekuwa tukililia kila siku kuwa tunatakiwa kuendesha mpira wetu katika sura ya “kibiashara”. Sura ambayo itamfanya mtu afikirie kuwa kwenda uwanjani kuwaangalia Simba na Mbao ni sehemu ya kutoka ” OUT” kwa ajili ya kuburudika na kutoa mawazo ya siku nzima.
Hatuwezi kufanya biashara sehemu ambayo hakuna amani hata kidogo. Ufinyu wa amani husababisha watu wengi kuogopa kwenda uwanjani kwa sababu tu wanaweza kudhulika kutokana na matendo yanayotokea ndani ya uwanja.
Mfano tukio la jana kwenye mechi kati ya Mbao na Simba, mashabiki wa Simba waliwashambulia wachezaji na baadhi ya viongozi wa timu kwa kuwatupia makopo. Jambo hili ni la hatari sana na alitakiwa kufumbiwa macho. Ni jambo ambalo linaturudisha nyuma kuamini kuwa mpira ni sehemu kubwa ya biashara na tunatakiwa kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara ya mpira wetu.
Mazingira ambayo vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu vihusishwe kwa kiasi kikubwa sana. Tunatakiwa tuwe makini kipindi mashabiki wanavyoingia uwanjani. Ni kukosa umakini mkubwa kuona shabiki anaingia na kitu ambacho kinaweza kutumika kama silaha ndani ya uwanja!. Polisi huingia kufanya nini kwenye hizi mechi??
Kuangalia mpira au kuhakikisha kuna mazingira salama kwa mtu yoyote kuangalia mpira kisha akaenda nyumbani kwao salama?. Tunaweza tukawa tunalaumu kila siku kuwa tunapata mapato kidogo kwenye mechi zetu, lakini kuna vitu huwa tunasababisha sisi wenyewe.
Tumekuwa na kasumba ya kuwaaminisha mashabiki wengi rangi nyeusi kuwa ni rangi nyeupe, ndiyo maana wanapopata nafasi ya kuona ukweli huwa wanapata hasira. Tuwe wakweli kwa mashabiki wetu, tusiwaaminishe kuwa tuna timu za kupambana na kina Lionel Messi wakati ni uongo.
Kuwa msemaji bora na kuhamasisha mashabiki siyo lazima kuwapa mashabiki wa timu yako uongo mtamu. Ni bora utumie ulichonacho kwa kusema ukweli unaoonekana ili kuepusha vitu ambavyo vinaweza kutokea kutokana na kuwaaminisha watu uongo.