Sambaza....

Mpira ni pesa, hii kauli ina maana kubwa sana ingawa sisi tunaichukulia kawaida kwa sababu tumezoea kuchukulia vitu kawaida katika ukawaida usio wa kawaida.

Mpira unatengeneza pesa nyingi sana kama ukiamua kuwekeza pesa , akili na muda kwenye mpira. Vitu hivi vitatu vina umuhimu mkubwa katika uwekezaji wa mpira biashara kwenye mpira ili upate faida.

Naaaam, faida ya kwenye mpira hupatikana kwa kuweka pesa, muda na akili ! . Hakuna kitu chenye mafanikio makubwa ambacho kinahitaji muda mfupi. Kila kitu chenye mkondo mkubwa wa mafanikio huitaji uwekezaji wa muda.

Ndiyo maana hata biashara ya kuuza wachezaji inahitaji muda, biashara hii haipo hapa Tanzania hasa hasa kwenye vilabu vyetu vikubwa. Wao walianzisha klabu kwa ajili ya kununua wachezaji tu, ni aghalabu kusikia Simba au Yanga imeuza wachezaji nje au ndani ya nchi kwa faida kubwa, hata ukisikia hiyo huwa ni bahati mbaya kwa sababu hakuna mipango ya kuonekana kwenye hii biashara.

Mzee Akilimali akiteta jambo na Manji

Hawana hata mascout ambao wangetumika kwa ajili ya kusaka vipaji vikubwa nchini ili waviendeleze kwa manufaa ya timu (ndani ya uwanja) na manufaa ya klabu ( kuwauza), wanategemea kugombania na Simba au Azam Fc pale Manungu. Hii ni vita ya watu wasio na akili ndiyo maana hawana hata mipango ya kuibua wachezaji vijana

Mipango yao ya kuibua wachezaji wenye umri mdogo kuanzia miaka sita (6) huishia kwenye karatasi na hakuna uhalisia wowote waliouonesha kupitia mipango yao.

Kuibua vipaji kutoka kwenye umri mdogo kuna faida kubwa sana kwa sababu vipaji hivi hukua katika mazingira ya msingi sahihi ya mpira, msingi ambao utawezesha kuwa na ukuta imara katika vipaji vya wachezaji na timu kwa ujumla. Mchezaji aliyekulia mazingira kama haya ni rahisi kumuuza nje na kupata pesa ndefu ambazo zitasaidia timu. Ni ngumu kukuta timu yenye mazingira ya kuuza wachezaji kuwa na vilio vya njaa. Na hiki kitu kinahitaji uwekezaji wa muda.

Uwekezaji wa muda huenda sambamba na uwekezaji wa akili. Unavyofikiria ndivyo unavyojitengeneza wewe mwenyewe.

Ulivyo sasa hivi ni matokeo ya ufikiriaji wako, unapoona muda huu Yanga inakosa pesa za miezi minne za kumlipa Mwalimu George Lwandamina ni matokeo ya ufikiriaji wa viongozi waliopita na wasasa.

Nembo yao ni kubwa mno kibiashara lakini wameshindwa kufikiria namna ya kuitumia nembo yao kibiashara ili iwe inaingiza pesa kubwa.

Kuna vitu vinaweza kuonekana ni vidogo lakini vina matokeo makubwa sana. Mfano, wapenzi wa Yanga ni watu wanaoipenda Yanga kutoka moyoni. Huwa wanaiunga mkono kwa hali na mali, lakini watu hawa hawajatengenezewa mazingira yatakayowafanya wao wanufaike na timu inufaike.

Wapenzi hawa wana familia ,ndani ya nyumba kuna vitu vingi sana vinahitajika ili vipendezeshe nyumba. Mlangoni pazia ni kitu cha msingi sana kwenye nyumba yoyote.

Yanga imeshindwa kuingia mkataba na wabunifu wa mapazia ambao watatengeneza mapazia yenye nembo ya Yanga. Hata kama mapazia haya yasipokuwa ya rangi ya njano na kijani , hata yakiwa na rangi nyeupe lakini yawe na nembo ya Yanga. Nembo shabiki wa Yanga atajivunia kununua, hawa watu tutawafanya wasiende kununua mapazia ambao hata hatujui yametengezwa na nani.

Zulia la mlangoni ni muhimu sana , ukiingia ndani utakutana na kapeti, kapeti ambalo litakuwa limebeba samani zenye nembo ya Yanga. Kiasi kwamba kuanzia kwenye zulia, kapeti, viti, kabati mpaka vikombe na sahani viwe na nembo ya Yanga.

Bidhaa hizi zinawafaa watu wenye hali ya juu na chini. Mazingira haya ukiwatengenezea utawapa nafasi ya kuzidi kukunufaisha wewe kupitia nembo yako kubwa. Na siku wakienda uwanjani watengenezee skafu, jezi na uwauzie, hili tushaimba sana.

Nafurahia muda huu wanaelekea kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa timu hii itasaidia timu iwe ze kujitegemea na kuachana na hulka ya kumtegemea mtu

Yanga kujiendesha kibiashara , kwa kujitegemea ni kitu chenye afya kuliko kuiendesha timu kwa kumtegemea mtu. Yusuph Manji kaondoka , timu imetetereka. Wachezaji hawalipwi mshahara, kocha kaondoka kwa sababu hajalipwa miezi minne.

Wafikirie na jinsi ya kuongeza wadhamini ambao watakuja kupunguza gharama za uendeshaji. Mfano wakiingia makubaliano na Gym ili wachezaji wake wawe wanafanya mazoezi ya Gym hii itakuwa na faida kwao Yanga na mmiliki wa Gym kwa kutangaziwa bidhaa yake. Kuna namna nyingi za kufikiria kibiashara kama akili yako ukiamua kuiwekea mwanga ndani yake na ukifanikisha hapo utakuwa umemtengeneza Manji wa kudumu kwenye klabu (mfumo imara wa mapato ya klabu) na kuachana na tabia ya kumtegemea mtu binafsi.

Sambaza....