Sambaza....

Kwa mara ya kwanza kumuona Ivan Zamorano ilikuwa ni kupitia picha yake kwenye sticker niliyoipata baaada ya kufungua big-g yangu.

Kwa wanaokumbuka enzi hizo mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni ya 2000 mpira wa ulaya ukiwa ndio unaingia kwa kasi, watoto wengi tulivutiwa na soka na hasa kupitia hizo stickers. Ilifika wakati unaenda kununua big-g ili tu upate kuona picha ya mchezaji. Nakumbuka sticker ya Ronaldo De Lima ndiyo ilikuwa adimu sana, ukiipata ni kama umepata dhahabu vile!

Nilikuwa najaribu kukuonesha jinsi mara ya kwanza nilivyoanza kumjua mtade huyu wa soka kutoka Santiago Chile. Ukiacha utaalamu wake ndani ya dimba kisa cha namba ya jezi yake kimeendelea kukumbukwa zaidi hadi leo.

Zamorano alitua Inter Milan mwaka 1996 akitokea Real Madrid na kukabidhiwa jezi namba 9 aliyoitumikia vyema.

Balaa likaingia mwaka 1997 Inter Milani ilipomsajili mfalme wa soka wakati huo Ronaldo De Lima Nazario akitokea Barcelona na kupewa uzi namba 10. Msimu wa kwanza walicheza kila mtu na jezi yake, mafanikio yalikuwa makubwa tu ndani na nje ya uwanja.

Msimu uliofuata kwa sababu za kibiashara ililazimika Ronaldo avae uzi namba 9 kwani jezi namba 10 haikuvutia wadhamini na mambo mengine ya kibiashara. Kumbuka kuwa taswira ya De Lima ilishajengwa kwa kuvaa jezi namba tisa na alishasaini mikataba mingi kwa namba hiyo.

Mambo yakawa moto! ikalazimika Zamorano aachie jezi namba tisa. Mkurugenzi wa michezo wa Inter Milani bwana Sandro Mazzola akamtaarifu Ivan kuwa anatakiwa aongeze namba nyingine mbele ya ile tisa, ili isomeke au 98, au 99 au namba yoyote kuanzia 91.

Zamorano aliipenda sana namba yake hivyo akamwambia bwana Mazzola kwani haiwezekani kuweka alama ya + kati ya 1 na 8 ili jumla iwe 9? Mazzola akamwambia amweleze Rais wa klabu, Massimo Moratti ambaye baadae alilitaarifu shirikisho la mpira Italia. Shirikisho liliridhia maombi hayo, Ivan Zamorano akaanza kuvaa jezi namba 1+8 ambayo kwa fikra zake aliona bado anaendelea kuvaa namba ya jezi aipendayo.

Henry Hamis 

Insta @henry_the_masive

Sambaza....