Sambaza....

Nyota wa Uhispania Andres Iniesta anatarajiwa kutangaza ndani ya siku mbili zijazo kujiunga na klabu ya Vissel Kobe ya nchini Japani baada ya kutangaza kustaafu katika klabu yake ya Barcelona.

Iniesta ambaye angeweza kukaa Barcelona licha ya umri wake kusogeza, anaweza kufuata njia ya mchezaji mwenzake Xavi ambaye naye alijiunga na timu nje ya Bara la Ulaya Al Sadd ya Qatar ili kukwepa kucheza na timu ya Barcelona.

Ilikuwa inafahamika hapo awali kwamba Kiungo huyo ambaye ni mshindi wa taji la Kombe la Dunia mwaka 2010 angejiunga na timu ya Chongqing Lifan ya China lakini uongozi wa klabu hiyo ulikanusha kuwa katika mipango ya kumsajili.

Kama akijiunga na timu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Japan (J-League) atakutana na mchezaji wa zamani wa Arsenal Lukas Podolski ambaye alijiunga na timu hiyo mwaka jana akitokea Galatasaray ya Uturuki.

Kwa sasa timu hiyo (Vissel Kobe) inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, nafasi ambayo Iniesta hajaizoea katika maisha yake yote ya soka akicheza Barcelona ambayo ametoka kuisaidia kutwaa mataji mawili msimu huu (Laliga na Copa del Rey).

Sambaza....