Kuna mengi sana yanazungumzwa mtaani, kuna vitu vingi sana vinaonekana kwenye klabu ya Yanga.
Vitu ambavyo vinatia huruma sana, kuna wakati unaweza kuwaonea huruma sana kipindi wanavyohangaika na Beno Kakolanya.
Wakati ukiendelea kuwaonea huruma kuhusiana na Beno Kakolanya , sikio lako litasikia tetesi kuwa kuna baadhi ya wachezaji wamegoma.
Na kuna habari huwa zinazagaa sana kuwa timu ya Yanga ina miezi kadhaa haijawalipa mishahara wachezaji wake.
Hapa ndipo unaweza kuchanganyikiwa na wakati mwingine kama ni shabiki wa Yanga unaweza kuchizika kwa sababu moja tu, nayo ni NJAA!.
Timu ina NJAA!, ndiyo maana habari nyingi zimeenea kwa timu kushindwa kuwalipa mishahara wachezaji hata kwa miezi 4.
Timu ina NJAA kwa sababu golikipa wao Beno Kakolanya anawadai pesa ya usajili tangu msimu jana.
Ndiyo maana kila uchwao yeye hugoma na huamua kucheza kipindi atakavyojisikia kucheza yeye. Ana kiburi kweli, na hiki ni kiburi cha kutafuta haki yake.
Haki ambayo anaitafutia sehemu ambayo kuna NJAA. NJAA ni msamiati mkubwa sana ambao umetawala katika eneo la Yanga.
Ni msamiati ambao siyo rafiki kabisa katika mazingira yetu ya mpira lakini ndiyo umejaa kwa wingi katika mitaa ya Jangwani.
Kwenye mpira kukiwepo na NJAA kuna hatari sana kwa timu kufanya vibaya. Kwenye mpira kukiwepo na NJAA hata morali ya wachezaji huonekana iko chini.
Lakini hiki kitu kiko tofauti kabisa na kikosi hiki cha Mwinyi Zahera. Kina NJAA kama inavyosemekana, hakijalipwa mishahara kwa muda mrefu.
Lakini ndicho kikosi ambacho kinafanya vizuri kwa sasa kwenye ligi kuu ya Tanzania bara kuliko kikosi kingine chochote.
Ndicho kikosi ambacho kina morali wa kupigana mpaka mwisho ili tu kipate matokeo chanya. Hawajawahi kukata tamaa.
Hata kwenye sare ambazo wamepoteza, walicheza kitimu. Walicheza kwa lengo moja tu, nalo ni kupata matokeo.
Hawakuweza kushinda dhidi ya Simba lakini walicheza kwa malengo ili kupata matokeo yoyote ambayo ni chanya kwao.
Mwanzo wa mchezo hadi mwisho wa mchezo akili za wachezaji huwa ndani ya uwanja na kusahau kila kitu ambacho huendelea nje ya uwanja.
Hakuna mchezaji ambaye anayekumbuka kuwa anadai mshahara wa miezi 4. Hakuna mchezaji anayekumbuka kuwa ana dai pesa yake ya usajili.
Akili zao hufikiria namna ambavyo watapata matokeo chanya ndani ya kikosi chao. Hawana mchezo wa kuvutia lakini wanamatokeo ya kuvutia.
Kwao wao hata kama wacheze mpira mbovu kiasi gani lakini matokeo yao yatakuwa mazuri sana. Na cha kushangaza wanaipigania timu yao utadhani wana hisa ndani ya hii timu.
Hawachoki dakika zote tisini, siwepesi kutoka mchezoni hata kama wakifanyiwa uonevu unaotokana na maamuzi ya refa. Kwao wao hutulia na kurudi mchezoni kwa ajili ya kucheza tu.
Hata kama wakitanguliwa kufungwa, huwa wanatulia na kuanza kutafuta goli la kusawazisha. Hakuna kinachowatoa mchezoni kabisa.
Mechi dhidi ya Tanzania Prisons walitanguliwa kufungwa lakini walitulia na kushinda magoli 3-1, tena dakika za mwisho.
Hii ni ishara tosha kuwa hawa huwa ndani ya mchezo dakika zote tisini, hata kwenye mechi ya jana dhidi ya Ruvu Shooting, walisawazishiwa dakika za mwisho ni.
Nilitegemea kuona Yanga ambayo imeghafirika kiakili na kupoteza utulivu baada ya wao kusawazishiwa lakini walitulia na kufunga goli la ushindi.
Na kina bonus gangs a zaidi kila mchezaji anayeingia kwenye kikosi cha Yanga huonesha kupigana sana. Mfano Yanga walimkosa Deus Kaseke hivi karibuni, lakini Jafary Idd aliweza kuziba pengo lake vizuri tu.
Gadiel Michael amekosekana kwa mechi kadhaa lakini pengo lake halionekani, jana Pius Buswita ameingia kwenye kikosi cha Mwinyi Zahera na ameonesha uwezo mkubwa.
Vyote hivi vinaonesha kuwa Yanga ina NJAA ya ubingwa na siyo ya pesa. Hakuna NJAA ya pesa kwenye miguu na mioyo ya wachezaji wa Yanga ina kuna NJAA ya UBINGWA.