Ligi haina mdhamini mkuu, hiki ni kitu ambacho kinaumiza kichwa sana. Ligi yenye timu 20, timu ambazo zinatoka katika mikoa mbalimbali, mikoa ambayo miundombinu yake siyo rafiki kwa kiasi kikubwa.
Miundombinu ambayo inafanya timu nyingi zipate gharama kubwa ya kuendesha timu. Makali ya gharama hizi yalitakiwa kupunguzwa kwa uwepo wa wadhamini.
Wadhamini ambao wangetoa pesa zao ili kuzisaidia timu. Lakini kwa sababu shirikisho la mpira nchini (TFF) halijui kuiuza ligi yetu ndiyo maana unaona ligi mpaka sasa hivi inakosa mtu wa kuidhamini.
Kitu hiki kinaweza kupunguza ushindani. Tumekuwa tukililia ushindani ndani ya ligi yetu. Tukiamini kabisa ushindani ndani ya ligi yetu itatufanya tupate bingwa imara.
Bingwa ambaye atatuwakilisha vyema katika mashindano ya kimataifa. Hii imekuwa tofauti kabisa, kila tukitamani kuusogelea msitari wa ushindani vikwazo vingi vinakuja mbele yetu.
Ndiyo maana hata suala la waamuzi limekuwa jambo ambalo linarudisha mpira wetu nyuma miaka yote.
Tunaweza kuorodhesha sababu nyingi sana ambazo zinasababisha mpira wetu usiweze kupiga hatua.
Juma anaweza kusema ukosefu wa viongozi wenye maono wanaokabidhiwa taasisi za mpira kuziongoza.
Mimi nikaja na sababu ya viwanja vibovu, mke wangu akaja na sababu ya kukosekana kwa makocha wenye uwezo wa kufundisha kwa ngazi za juu.
Huku mtoto wangu akalalamika kuhusiana na ukosefu wa vituo vya kuibua, kulea na kukuza vipaji.
Lakini pamoja na sababu zote hizo ikakosekana sababu ya waamuzi. Hii ni moja ya sababu ambayo inatufanya tupige hatua nyingi za kurudi nyuma. Kuna maamuzi ambayo hufanyika ndani ya uwanja yanakera sana!.
Kuna wakati mwingine waweza kutokwa na tusi kubwa mdomoni kwa sababu ya maamuzi ambayo yanatokea ndani ya viwanja.
Ni aibu kwa chama cha waamuzi Tanzania, kuna haja gani ya kuwa na chama kama hiki kama kinatoa waamuzi ambao wanatoa maamuzi ya kuzinyonya timu nyingi?
Timu nyingi zinatumia muda mwingi na fedha nyingi kwa ajili ya kuziandaa timu.
Badala ya matokeo kupatikana kutokana na kuzidiwa kwa mbinu kwa timu fulani lakini matokeo hupatikana kutokana na utashi wa waamuzi wengi.
Wamekuwa wakiziua timu nyingi kwa kushindwa kuzitafasri vyema sheria za mpira wa miguu.
Sehemu ambayo siyo mpira wa kuotea (Offside) kwao wao huamua kuwa ni mpira wa kuotea (offside).
Sehemu ambayo ni mpira wa kuotea (offside) kwao wao huwa siyo offside.
Hakuna haki inayotendeka ndani ya uwanja. Na inawezekana kabisa mafunzo ambayo hupitia huwa hayana msaada mkubwa sana.
Kuna haja ya kuendesha mchujo wa waamuzi kwa ufasaha. Majaribio yanayofanyika kuwapata waamuzi ni majaribio ya muda mfupi sana.
Hata mwamuzi husika hupata nafasi ya kuchezesha ligi kuu Tanzania akiwa hajakomaa vya kutosha , kwa sababu hutumia miaka michache kuchezesha ligi za madaraja ya chini kabla hajapanda.
Kipimo sahihi na bora ni kwa waamuzi kutumia muda mwingi wakichezesha ligi za madaraja ya chini huku wakifuatiliwa kwa ukaribu kabla hawajapandishwa kuchezesha ligi kuu ya Tanzania.
Ligi kuu ni eneo kubwa, eneo lenye ushindani mkubwa na ni eneo ambalo macho ya wengi hutazama kinachoendelea uwanjani, hivo kukosea kwako kwa kosa moja unakuwa umekatiri mioyo ya watu wengi.
Chama cha waamuzi wa soka Tanzania kinatakiwa kuweka misingi bora ya kuwapata waamuzi hawa ili kupata waamuzi ambao watatenda haki katika ligi zetu.
Kama kweli tunataka kupata mshindi halali kwenye ligi yetu, mshindi imara ambaye atatuwakilisha vyema katika mashindano ya kimataifa, inabidi chama cha waamuzi Tanzania watusaidie kupata waamuzi bora.
Ligi yenye waamuzi bora ndiyo ligi bora inayotoa mshindi bora, waamuzi wanamchango mkubwa sana wa kukuza na kudumaza soka letu .