Inawezekana baada ya vilabu vya Uhispani kutawala kwenye ligi ya Mabingwa Ulaya kwa zaidi ya mwongo mmoja kwenye hatua ya robo fainali, Mwaka huu tukashindwa kabisa kuiona miamba hiyo ya soka kwenye hatua hiyo muhimu.
Baada ya Valencia kuondolewa kwenye hatua ya makundi, tumeshuhudia Real Madrid wakitolewa na Ajax kwa kichapo cha nyumbani cha mabao 4-1 (Agg 3-5), huku jana pia Athletico Madrid ambao walikuwa na matumaini ya kupenya baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani kwao kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wakifungwa mabao 3-0 na Juventus na kuondolewa mashindanoni.
Mpaka sasa imebaki timu moja pekee ambaye ni Barcelona ambaye naye kama mambo yatakwenda vizuri na kupata ushindi basi itakuwa timu pekee kutoka uhispania kupenya kwenye hatua ya robo fainali, Barcelona atawakaribisha Lyon ya Ufaransa na kumbuka katika mchezo wa awali walitoka sare ya 0-0.
Ni jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka kuona kama kuna timu yoyote ya Uhispania itapenya kwenye hatua ya 16 bora na kutinga robo fainali, ukizingatia kwa miaka 10 sasa timu za Uhispania ndizo ambazo zimetawala ligi hii wakichukua kwa ujumla mataji 7 (Barcelona matatu na Real Madrid manne).
Mpaka sasa timu ambazo zimefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ni pamoja na Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur zote za England, Juventus ya Italy, Ajax ya Uholanzi na Porto ya Ureno, zikibaki nafasi mbili ambazo zitafahamika leo pale Bayern Munich atakapocheza na Liverpool na Barcelona akiwakaribisha Lyon.