Timu tatu zilizopanda daraja msimu huu ni klabu mpya ambazo hazijawahi kuonja ladha ya Ligi Kuu Bara, Dodoma fc, Gwambina fc pamoja na Ihefu fc wamepanda kushiriki Ligi Kuu Bara.
Haikua rahisi kwa Ihefu kupanda Ligi Kuu, baada ya kufanya vizuri katika michezo ya Ligi daraja la kwanza na kumaliza nafasi ya pili kundi B ililazimika kucheza “Playoffs” dhidi ya Transit Camp na kufanikiwa kuvuka na kwenda kukutana na Mbao fc ya Mwanza pia na kufanikiwa kuwatoa na kupanda Ligi Kuu Bara.
Baada ya kupanda Ligi Kuu Bara moja ya usajili wa maana walioufanya ni kunasa saini ya kiungo John Mbise dakika za usiku kabisa kutoka Namungo fc. Tovuti ya Kandanda ilipata wakati wa kuzungumza na kiungo huyo mpya wa Klabu ya Ihefu fc baada ya kukamilisha dili lake hilo.
Mbisse mchezaji wa zamani wa Dodoma fc na Mshikamano amezungumzia mengi ikiwemo malengo ya binafsi na ya klabu kwa ujumla katika msimu huu wa 2020/2021.
John Mbise “Kwanza kabisa nafurahi kuwa katika klabu yangu mpya ya Ihefu baada kufanikiwa kujiunga nao dakika za usiku kabisa kabla ya dirisha halijafungwa. Binafsi kama mchezaji nimejiandaa vizuri pia timu ina wachezaji wazuri na mimi nimejipanga kuleta changamoto na kuhakikisha napata nafasi ya kucheza nafasi ya kucheza.
Nafasi ya kucheza naiona ipo ila kunahitaji kupambana na kuonesha uwezo wa hali ya juu ili kuaminika kwa kocha na kunipa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.”
Kiungo huyo aliepitia Simba B pia amezungumzia ugeni wa klabu yao ya Ihefu katika Ligi lakini wamejiandaa kutoa ushindani haswa, lakini pia akazungumzia malengo ya klabu yake na malengo binafsi kama mchezaji.
“Pia kuhusu timu ndo mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu inaonesha italeta ushindani mkubwa hivyo tutarajie mazuri kwenye hii timu. Sisi kama klabu tunajiandaa kushika nafasi nne za juu licha ya ugeni wetu katika Ligi.
Malengo yangu kama mchezaji ni kucheza vizuri kuonesha uwezo wangu niweze kupata timu kubwa zaidi ya hapa nilipo au kucheza nje ya nchi na kuitumikia timu yangu ya Taifa.”
John Mbise pia hakusita kutoa sababu zilizomfanya kuondoka katika timu ya Namungo fc.
“Namungo ni timu nzuri lakini niliamua kuondoka kule Ruhangwa na kuja kutafuta changamoto mpya, na ndio maana unaniona hapa Ihefu leo.”