KIUNGO mshambulizi wa Yanga SC, Ibrahim Ajib ameanza msimu wa ligi kuu Tanzania Bara kwa kuhusika katika magoli matano kati ya saba yaliyofungwa na timu yake katika michezo mitatu waliyokwishacheza.
Ajib aliingia uwanjani kama mchezaji wa akiba katika robo saa ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar FC siku ya ufunguzi wa msimu- 24 Agosti na kuonyesha kiwango cha juu katika mchezo walioshinda 2-1 ndani ya uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha Zahera Mwinyi mara kadhaa amekuwa akisema, Ajib ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na kama atajibidiisha atafika mbali kimpira.
゛Ndiyo, nafahamu kocha anahitaji nini kutoka kwangu. Amekuwa akinisisitiza kujituma uwanjani na kufanya vizuri katika mazoezi. ゛ anasema Ajib.
Michezo miwili iliyopita:
04/11/2017 | Singida United | 0 – 0 | Young Africans SC |
11/04/2018 | Young Africans SC | 1 – 1 | Singida United |
Namba 10 huyo alianzishwa katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa pili wa Yanga msimu huu na ndani ya dakika saba za mwanzo aliweza kumtengenezea Mrisho Ngassa goli, akafunga na kumtengeneza magoli mengine mawili kwa mlinzi wa kati Vicent Andrew na kiungo Deus Kaseke katika ushindi wa 4-3 dhidi ya Stand United.
゛Najisikia vizuri zaidi pale ninapocheza vizuri na kuisaidia timu yangu kushinda mechi. Wakati mwingine inaumiza kuruhusu magoli mengi katika mchezo mmoja, lakini niwaambie tu mashabiki wetu kilichotokea katika mchezo wetu dhidi ya Stand ni uhalisia wa mchezo wa soka. Muhimu ilikuwa kupata matokeo lakini tutajitahidi kufanyia kazi makosa yetu mechi hadi mechi.゛anasema Ajib.
Jumatano hii Ajib aliendeleza kiwango chake kizuri wakati alipopiga pasi ya mwisho iliyozaa goli pekee la Heritier Makambo katika ushindi wa Yanga 1-0 Coastal Union na kuifanya timu yake kushinda mara tatu mfululizo kabla ya mchezo wa usiku wa leo dhidi ya Singida United.
“Tunacheza kitimu, hata kama hatujafikia kiwango cha juu zaidi lakini tupo ndani ya malengo yetu. Kushinda mechi ndio malengo yetu makubwa bila kujali tunachezaje. Tunataka kuifunga Singida, kisha Simba. ゛anasema mchezaji huyo aliyetemwa timu ya Taifa.
Singida United haikupoteza mchezo wowote dhidi ya Yanga kati ya michezo mitatu waliyokutana msimu uliopita. Mechi ya kwanza ya ligi matokeo yalikuwa suluhu-tasa katika uwanja wa Namfua, Yanga ikapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalty katika robo fainali ya FA mechi ambayo ilimalizika 1-1 katika dimba la Namfua, mchezo wa tatu uliisha 1-1 katika uwanja wa Taifa.
“Hatuangalii yaliyopita, ni kweli Singida walitusumbua sana msimu uliopita, lakini licha ya kuendelea kuwaheshimu wanatakiwa waelewe kuna mengi yamebadilika katika timu zote. Tunahitaji kushinda dhidi yao ili tuongoze ligi Kuelekea mchezo dhidi ya Simba.゛
Je, amelipa Yanga? “Msimu wangu wa kwanza hapa haukuwa mzuri sana kutokana na kiwango cha kupanda na kushuka. Zahera ni mwalimu mzuri na naamini nitafanya vizuri zaidi msimu huu ili kufikia malengo ya klabu. Naamini nitaendelea kunyanyua kiwango changu na nitaacha kazi yangu izungumze.”