Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dr Harrison George Mwakyembe ameitaka klabu ya soka ya Yanga kuheshimu maelekezo ya serikali ya kuitaka klabu hiyo kufanya uchaguzi ili kuziba nafasi za viongozi zilizoachwa wazi.
Mwakyembe amesema licha ya taarifa za mkanganyiko zinazotoka ndani ya klabu hiyo kwamba aliyekuwa Mwenyekiti kabla ya kujiuzulu Yusuph Manji kurejea lakini ni lazima klabu hiyo kufanya uchaguzi kama walivyokubaliana na shirikisho la soka nchini (TFF) na baraza la michezo la Taifa (BMT).
“Serikali tulishatoa maelekezo kwa baraza la michezo la Taifa, utekelezaji umeshaanza yale tuliyoyaamua, imeelekezwa kwa Shirikisho la soka na imewekwa tarehe 15 mwezi wa kwanza kuwa uchaguzi ndani ya Yanga kuziba nafasi, ni kwa mujibu wa Sheria”
“Hatuwezi kuwa na sheria mbili, moja ya Yanga na nyingine ya vilabu vingine, huo ndio msimamo ninaoujua, mengine yanayoongelewa huko pembeni sijui leo Manji ameamka vizuri au vibaya….. hayo ni mambo yenu wenyewe huko, ninachojua nimetoa maelekezo na sijapata mrejesho kwamba kuna matatizo yoyote yale, lazima Yanga ijaze hizo nafasi kwa Mujibu wa Sheria” Mwakyembe amesema.
Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Baraza la Wadhamini Yanga, kupitia kwa Mwenyekiti wake, George Mkuchika, kusema Manji ameandika barua ya kuomba kurejea kwenye nafasi yake hivyo hakuna tena haja ya kujaza nafasi ya Uenyekiti.
Tayari kuna taarifa kwamba Thobias Langalanga ambaye alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, kwamba ameamua kujivua wadhifa huo jana.
Langalanga ameamua kujivua kutokana na kurejea kwa Yusuf Manji ambaye alitangaza kujizulu takaribani mwaka mmoja na miezi kadhaa sasa imepita.
Kujivua kwa Langalanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kumemfanya afunguke kuwa yeye anamkubali Manji hivyo hana haja ya kuendelea kushikilia nafasi hiyo.
Na tayari Kamati Tendaji ya klabu ya Yanga imeitisha mkutano wa dharura ambao umepangwa kufanyika Novemba 24 huku mahali pa kukutana kukiwa bado hakujatangazwa.
Kuelekea uchaguzi wa Yanga utakaofanyika January 15, 2019, Yanga itafanya uchaguzi wa kujaza nafasi zingine zilizo wazi ikiwemo baadhi ya nafasi za Kamati ya Utendaji, Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti.