Katibu Mkuu wa klabu ya soka ya JKT Tanzania Abdul Nyumba amesema hawajapokea barua rasmi kutoka Bodi ya Ligi ikionesha mabadiliko ya mechi yao na Yanga kupigwa uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Nyumba amesema wanachofahamu wao kuwa mechi ya Novemba 26 ni mechi ya kiporo na inatakiwa kuchezwa katika uwanja wa Mkwawani Jijini Tanga na si uwanja wa Taifa Kama ambavyo wameendelea kusikia kwenye vyombo vya habari.
Amesema Kama mchezo huo utapigwa kwenye uwanja wa Taifa basi ni vyema Bodi ya Ligi wakaonesha ni kipengele kwenye kanuni za Ligi ambacho kinaruhusu mechi ya raundi ya pili kuchezwa raundi ya kwanza au kuonesha wazi mechi hiyo nani anapaswa kuwa mwenyeji.
“Kimsingi sisi hatuna matatizo na Yanga isipokuwa Bodi ya Ligi wanashindwa kuweka wazi haya mambo, wao wanadai wamefanya marekebisho ya Ratiba katika uwiano wa mechi za nyumbani na ugenini, lakini suala hili sidhani kama lina utata kwa maana mechi yetu hii ni ya kiporo, Bodi ya Ligi ilipanga tarehe hizi ni kwa ajili ya mechi za kiporo, wanatakiwa kucheza na sisi Kama mechi ya kiporo ambayo ilitakiwa kifanyika tarehe 26,”
“Lakini Bodi ya Ligi inatumia mwanya huo, kusema walishafanya marekebisho, sisi hatujapata barua hiyo, Kama barua rasmi, Kama wanataka kufanya tofauti basi wanatakiwa kusema kinagaubaga Kuwa mechi hii ni ya raundi ya pili na Sio ya kiporo hapo Tutaenda kucheza Taifa,” Nyumba amesema.
Ikumbukwe tayari JKT Tanzania walishafanya Mabadiliko ya mechi za nyumbani kwa timu za Simba na Yanga, ambapo walichagua uwanja wa Mkwawani Jijini Tanga kutumika kwa mechi hizo Lakini kwa siku za Hivi karibuni kumeibuka sintofahamu Baada ya taarifa kuzagaa ikisema Bodi ya Ligi imeurejesha mchezo huo kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.