Sambaza....


WAKATI wachezaji na benchi la ufundi wakiendelea ‘kusotea’ mishahara yao kwa mwezi wa tatu sasa, uongozi wa Mbao FC upo katika mipango ya kumuongeza kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Ally Bushiri ‘Benitez’ ili kusaidiana na kocha wa sasa Amri Said ‘Stam’

Mwanzoni mwa mwezi huu, uongozi wa Mbao FC uliwalipa wachezaji wake pesa zao za usajili lakini mambo bado yanakwenda ‘mrama’ kutokana na benchi lote la ufundi kudai mishahara kwa miezi mitatu sasa sambamba na wachezaji.

“ Hali ya kiuchumi ni mbaya mno katika klabu ya Mbao. Wachezaji licha ya kwamba walilipwa pesa zao za usajili walizoahidiwa wakati wakijiunga mwezi Juni, mishahara yao na benchi la ufundi imekuwa tatizo na ninavyokwambia ni kwamba uongozi unafikiria kumuongeza kocha Bushiri ili asaidiane na Stam.”

Mbao imshindwa kupata ushindi katika michezo mitano iliyopita na sababu kubwa imekuwa ikitajwa ni wachezaji kupoteza morali yao ya mchezo. Kuongezwa kwa Bushiri kunaweza kuwa na nafuu lakini ni lazima uongozi wake utazame kuhusu madai ya mishahara yanayowakabili.

“ Amri alitaka kuondoka mwezi uliopita, na ni yeye aliyelazimisha uongozi uwalipe pesa zao za usajili wachezaji. Naye ni kama amechoka kwa ahadi zisizokwisha na nasikia amewaambia viongozi yupo tayari kuondoka na amewataka kama watamleta Bushiri basi aje na wasaidizi wake ili yeye akae pembeni. Kwa kweli hali jinsi ilivyo na kama hakutafanyika maamuzi ya busara naona timu ikiwa hatarini zaidi katika ligi.” Kilimaliza kusema chanzo cha habari hii.

Sambaza....