Sambaza....

Jina lake lilianza kuwa maarufu katika masikio yetu kwenye kipindi cha usajili, usajili wake ulikuwa wa ajabu ajabu!.
Ila haikuwa ajabu kwa masikio na macho yetu kushuhudia mambo ya ajabu ajabu katika mpira wetu kwa sababu tumezoea na tunapenda sana kufanya mambo ya ajabu ajabu.
Uajabu huu ndiyo umetufiksha hapa tulipo, ndiyo maana kwa mara ya kwanza tulitangaziwa kuwa Faisal “Toto” ameshamalizana na Singida United na hata kutambulishwa akatambulishwa lakini kesho yake tulimuona akiwa na jezi ya Yanga pamoja na kiongozi wake wa JKU akitangazwa kama mchezaji wa Yanga!.
Huu ndiyo uajabu ambao ni vigumu kuuvumilia ila sisi tumeshauzoea na huwa tunauvumilia na kuendelea kuishi ndani yake.
Hatuoni haya, wala mashimo ya pua zetu hayasikii harufu yoyote ya uajabu ambao tumezoea kuufanya katika mpira wetu.
Kwetu sisi mpira tunafanya kama mazoea, neno kufanya mpira kama kazi halipo kabisa katika mishipa ya damu yetu!, tupo tupo tu!, hatueleweki tunaenda kulia au kushoto, nyuma au mbele!.
Kukoswa kwetu mwelekeo ndiyo kumesababisha leo hii Haruna Moshi “Boban” akiwa pale African Lyon akionekana kama mchezaji wa kawaida sana.
Hatishi nje ya uwanja!, hana kitu kikubwa nje ya uwanja cha kuwafanya wenzake pale African Lyon wapigane kwa nguvu ili na wao waje kufanikiwa kimaisha kama yeye.
Siyo mfano bora kabisa wa kumtolea mtu kipindi unapompa somo la mpira ni kazi!, atakuelewaje !?, utamshawishi vipi akuelewe kuwa mpira ni kazi kubwa inayoingiza kipato wakati kipaji kikubwa kilichowahi kutokea hapa Tanzania kama Haruna Moshi “Boban” hakijafanikiwa sana kimaisha?.
Ilitakiwa Haruna Moshi “Boban” awe anaingia na gari yake yenye gharama kubwa katika mazoezi ya African Lyon. Tena wakati huo amewaacha mafundi wakiendelea kujenga hekalu lake la kifahari.

Hata kipindi ambacho wachezaji wa African Lyon wangelia kutolipwa posho yeye ndiye angesimama kama mkombozi wa mwisho kuwalipa hizo posho. Tumeshashuhudia mara nyingi sana hiki kitu!, kina Samuel Etoo wameshahusika sana kutoa posho kwenye timu zao za taifa kipindi ambacho wachezaji wa timu ya taifa walipogoma kisa kutopewa posho.

Huu ndiyo mfano bora sana wa kuutumia kwenye somo la “Mpira ni kazi kubwa inayolipa sana”. Huwezi kutolea mfano wa Haruna Moshi ” Boban” kwenye somo hili licha ya kwamba alikuwa na kipaji kikubwa sana enzi za ujana wa miguu yake.
Kuna vipaji vingi sana vinavyokufa vikiwa masikini kila uchwao, na hii ni kwa sababu tumezoea kuishi katika nchi ya ajabu kabisa. Nchi inayopenda uajabu ajabu usiokuwa na faida yoyote kubwa.
Nchi ambayo haijali vipaji vikubwa, nchi ambayo wachezaji wengi hawajielewi, hawana dira katika maisha yao ya mpira, hawajui wanataka nini , wanachokifanya wao ni kukimbia kwa kasi bila uelekeo.!
Wanakimbia ilimradi tu waonekane wanakimbia, na kibaya zaidi hawana hata washauri bora, wamezungukwa na watu ambao hawawashauri vizuri, watu ambao hawawatii hasira ya kufanya kitu kikubwa katika maisha yao.
Na ambavyo hawana elimu pamoja na malengo , wachezaji wetu hawajawahi hata siku moja kuwa na wasimamizi bora wa vipaji vyao. Wasimamizi ambao watawaongoza na kuwakumbusha adhima ya wao kuvaa jezi ya timu fulani na viatu vya mpira.
Wasimamizi ambao watawakumbusha kuwa jua la kesho asubuhi halitakiwi kuwakutia Tanzania. Sehemu ambayo haina fedha, sehemu ambayo ilimfanya Haruna Moshi “Boban” kumaliza maisha yake ya soka akiwa hana kiasi kikubwa cha fedha.
Sehemu ambayo inapenda vitu vya ajabu, na ndiyo sehemu ambayo Said “Khamis” Ndemla ameipenda sana na hataki kuondoka na ameshasahau kabisa kuwa ana kipaji ambacho hakitakiwi kuwa hapa Tanzania.
Sehemu ambayo leo hii tunamshuhudia Faisal “Toto” akikabidhiwa umiliki wa dimba la Yanga. Tena akaaminiwa sana!, na kibaya zaidi kapewa mzigo mzito mgongoni mwake ilihari miguu yake haijakomaa kuhimili uzito wa mzigo huo!, tuachane na hayo!. Turudi hapa kwa Ndemla na Faisal.
Hakuna ambaye hajui kuwa hawa wana vipaji vikubwa sana, na kikubwa zaidi Said Ndemla aliwahi kutoka kabla ya Faisal, na alikuwa anapata nafasi nyingi sana za kufanya majaribio nje ya nchi. Lakini akawa anarudi nyumbani bila majibu mazuri ya kutushawishi sisi.
Hakutaka kuwa muwazi, nahisi ndiyo sababu ya yeye kuendelea kuwepo hapa , sehemu ambayo hastahili kuwepo, lakini bado yupo na kuna dalili kubwa ya yeye kuwepo hapa na inawezekana mwisho wake utakuwa kama wa Haruna Moshi “Boban” , huwezi jua!, lakini waliosema dalili ya mvua ni mawingu hawakuwa wamekosea hata kidogo!.
Mahesabu yetu yanaonesha tunaenda kumpoteza tena Said “Khamis” Ndemla. Maajabu ya hesabu siku zote, wakati unatoa utaletewa kujumuisha.
Tushaanza kumjumuisha Faisal katika mpira wetu kama mchezaji ambaye ana kipaji. Lakini hofu yangu ya uajabu wa nchi yetu na huyu kuna uwezekano mkubwa hadithi yake tutakuja kuisimulia kama ambavyo tunaisimulia hadithi za Haruna Moshi “Boban” na Said Ndemla kama tu hatoamua kuwa na wasimamizi bora na wazuri wa kipaji chake na kuisahau dira ya maendeleo yake ya mpira. Hasira, upambanaji wenye malengo, juhudi, nidhamu na maarifa vinatakiwa vivae ngozi ya mwili wake!.

Sambaza....