Kutengeneza hela ni sanaa, kufanya kazi ni sanaa ila kufanya biashara ni sanaa kubwa zaidi
Kuna biashara nyingi sana kwenye tasnia ya michezo lakini hatujawahi kuzifanya katika kiwango kikubwa cha ubora.
Ukawaida usio wa kawaida umetawala sana kwenye eneo hili la biashara za michezo, ndiyo maana mafanikio yetu ya kawaida ndani na nje ya uwanja
Hatujawahi kuumizwa na utajiri wanaopata wenzetu kutokana na kufanya biashara ndani ya tasnia ya michezo
Tasnia ambayo ina idadi kubwa ya watu wanaoipenda na kuifuatilia, idadi ambayo inatoa taswira halisi ya soko kubwa la biashara hili.
Soko ambalo tunalichukulia kawaida na kuliangalia tu siku ya mechi.
Tunategemea siku ya mechi ndiyo iwe siku ambayo tutatengeneza pesa nyingi na kusahau kuwa hata kabla ya mechi tunaweza kutengeneza pesa kupitia michezo.
Siku ya mechi ya Simba na Al Masry kuna mengi yalitokea, lakini moja ya jambo ambalo lilinishtua binafsi na kunifanya niliangalie katika upande tofauti na wengine walivyokuwa wanalitazama ni suala la mashabiki kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) na kuanza kuteleza wakati mvua inaendelea kunyesha.
Inawezekana wengi wetu tulikemea tabia ile, hata mimi nilikemea kwa sababu ni tabia mbaya ambayo inahatarisha afya ya uwanja wetu.
Tujiulize kitu kimoja, kukemea peke yake na kunyamaza kunatosha? , sawa tunaweza tukawa tumekemea na kuwafanya mashabiki wasirudie tena tabia ile.
Je tunatakiwa kuishia kwenye kukemea tu ? Hivi hatukuona furaha iliyokuwa imetanda kwenye nyuso za mashabiki wakati wanateleza kwenye ule uwanja? tunafanya nini ili kuweka furaha ya kudumu kwenye nyuso za mashabiki wale?
Kama watu wanapenda kitu watakusikiliza, lakini kama watu wanakuamini watafanya biashara na wewe, kuna umuhimu mkubwa sana ya kujenga imani kwa hawa watu ili waweze kufanya biashara na nyie.
Hapa kuna vitu viwili vya kufanya ili kuweka imani kubwa ndani ya watu ili kutengeneza mazingira rafiki ya kibiashara
Cha kwanza, ni kuwakemea hao watu walioenda kwenye sehemu ya kuchezea ( pitch) na kuanza kucheza wakati mvua inanyesha
Eneo hilo la kuchezea (pitch) sportpesa wametumia bilioni 2 kutengeneza eneo la kuchezea (pitch) lenye hadhi ya kimataifa
Bila utunzaji mzuri wa hii pitch tutabaki kusema tuliwahi kuwa na pitch ya hadhi ya juu ya kimataifa
Wasimamiza wa uwanja wanatakiwa waweke ulinzi ambao utalinda miundo mbinu ya huu uwanja.
Jambo la pili, ni kuuendesha kibiashara huu uwanja. Ni wakati ambao wasimamizi wa uwanja wasisubiri viingilio vya mechi kwa ajili ya kupata pesa za utunzaji wa huu uwanja.
Kama ilivyojionesha kwenye mechi ya Simba na Al-Masry kuna watu wana ndoto ya kukanyaga kwenye hiyo pitch. Kuna watu kutoka mikoani ndani ndani huko ambao wanatamani kutoa tongotongo zao kwa kukanyaga hiyo pitch , inabidi watengenezewe mazingira ya kibiashara, mazingira ambayo yatawawezesha wao kuja kufanya utalii kwenye uwanja huo na kukanyaga pitch kwa gharama elekezi.
Pia kunaweza kujengwa maktaba ya iliyo na machapisho ya wachezaji wetu wa sasa na wazamani kuelezea historia yao. Mtu akija awe na uwezo wa kupata historia ya Sunday Manara na wachezaji nyota wa zamani na sasa akimaliza hapo aende kupiga picha kwenye pitch , ateleze apendavyo, kuwepo na mipira ambayo ataitumia kupiga penalti akimaliza hapo aende na kwenye majukwaa
Kwenye makumbusho ya Taifa kuna vitabu na picha zinazohusu timu ya taifa na wachezaji wa zamani pamoja na makombe ambayo Taifa Stars iliwahi kushinda
Vitu kama hivi vinatakiwa vipelekwe pale Uwanja wa Taifa. Iwe chachu ya utalii wa uwanja kuwepo na maktaba maalumu ya vitu hivo
Maktaba ambayo itakuwa mpaka na CD ambazo zitakuwa na mahojiano ya wachezaji nyota wa zamani. Vijana wengi hawajui historia za wachezaji wao wa sasa na zamani, tunatakiwa tuwatengenezee mazingira ya kibiashara ili na wao wanufaike
Kuna nyota wengi sana ambao walileta sifa kwenye taifa hili kwenye michezo mbalimbali kama soka, riadha, ngumi na michezo mingine.
Watu wengi wanahamu ya kuwajua kiundani hawa watu waliofanya vizuri, hivo kutengeneza mazingira mazuri ya watu mbalimbali kupata historia zao itaongeza chachu ya watu kwenda kutalii kwenye uwanja wa taifa
Pia hata kuwajengea sanamu za heshima na kuziweka kwenye maktaba maalumu au nje ya uwanja itaongeza chachu ya watu kujivunia mashujaa wao