Mlinzi wa zamani wa Tanzania Prisons ya jijini Mbeya David Mwantika ni kama amekua hasomeki hivi tangu alipotoka kushiriki na timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” katika michuano ya Afcon iliyofanyika nchini Misri mwaka jana.
Mwantika ambae alikua ni kipenzi cha mwalimu wa timu ya Taifa wakati huo Emmanuel Amunike alijumuishwa katika kikosi cha Stars dakika za mwisho baada ya mlinzi mwenzake wa Azam fc Agrey Morris kupata majeraha ya goti katika mchezo wa mwisho wa kirafiki wa Stars.
Baada ya uteuzi wa mwalim Amunike wa kumpa nafasi Mwantika kuziba pengo la Morris wadau wengi walikosoa uteuzi wake na hivyo mashabiki wengi wa soka wakaonyesha wazi kutokukubaliana na uchaguzi mzima wa timu ya Taifa.
Baada ya michuano kuisha na Tanzania kupoteza michezo yote mitatu na kumaliza wamwisho katika kundi chini ya Kenya, Senegal na Algeria kibarua cha Mnigeria Emmanuel Amunike kilikatishwa na hivyo mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona kufuzwa kazi na nafasi yake kupewa Ettiene Ndayiragije raia wa Burundi..
Tangu michuano hiyo ilipoisha Mwantika amekua hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Azam fc na kushindwa kujihakikishia nafasi mbele ya Agrey Morris, Yakubu Mohamed na Oscar Masai. Hii ilipelekea Mwantika kuonekana kwa nadra na jezi ya Azam katika msimu wa 2019/2020.
Baada ya kukosa nafasi klabu ya Azam fc katika dirisha dogo iliamua kumtoa kwa mkopo kwenda katika klabu ya Lipuli fc Iringa lakini Mwantika hakujiunga na klabu hiyo. Baada ya Mwantika kutia ngumu kwenda kujiunga na Lipuli hajaonekana uwanjani mpaka leo na kupelekea kumaliza karibu nusu msimu akiwa nje bila klabu.
Inasemekana bado wapo katika mzozo na klabu yake ya Azam fc ili kumalizana kila upande ubaki salama na chake, hivyo huenda msimu ujao Mwantika akaonekana na klabu nyingine hapa nchini ama nje ya nchi.