Klabu ya soka inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni KMC FC maarufu kama “Kino Boys” ni kama historia ipo upande wao katika michuano ya Azam Sports Federation Cup.
Baada ya kuiondosha kwa mabao mawili kwa sifuri African Lyon katika uwanja wa Jenerali Isamuhyo Mbweni sasa KMC inasubiri mshindi kati ya Kagera Sugar ama Azam f c ili kucheza nae nusu fainali.
Alikua ni Mohamed Rashid na Cliff Buyoya walioipeleka “Kino Boys” nusu fainali huku mabao yote mawili yakitengenezwa na Omary Ramadhani “Berbatov”
Tangu michuano ya ASFC ianze mwaka 2017 chini ya udhamini wa Azam tv timu zilizopanda daraja zimekua na bahati ya kufika fainali ya michuano hiyo, lakini wamekua wakifungwa na Klabu kongwe za Ligi Kuu.
Katika msimu wa kwanza mwaka 2016/2017 fainali ilipigwa Dodoma katika dimba la Jamuhuri na kuikutanisha Mbao fc dhidi ya Simba. Lakini Mbao fc ililoa mbele ya Simba sc kwa kupigwa bao mbili kwa moja.
Katika msimu wa pili 2017/2018 ilikua ni zamu ya Singida Utd iliyokua imepanda daraja ambapo ilikutana na Mtibwa Sugar katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Ndoto za Singida utd zilizimwa na Salum Kihimbwa katika dakika za jioni kabisa na kuifanya Mtibwa kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa mawili.
Katika msimu huu sasa ni zamu ya KMC kuendeleza rekodi ya timu zilizopanda daraja kucheza fainali ya Azam Sports Federation Cup.
Je KINO BOYS watafanikiwa?, Tusubiri tuone!