Sambaza....

Niliwahi kuandika kuwa ni ngumu kwa Yanga kubeba ubingwa wa ligi kuu ikiwa na mshambuliaji aina ya Makambo. Na hii ni kwa sababu anakosa nafasi nyingi sana za wazi. Na kibaya zaidi hakuna mtu ambaye anaweza kuwa kama mbadala, benchi la Yanga lina ufinyu wa washambuliaji, ufinyu ambao unamfanya Makambo kuwa kama mshambuliaji pekee katika klabu ya Yanga.

Kwa hiyo yeye anatakiwa aibebe Yanga, kwa sababu yeye ni mhimili mkubwa. Yanga haipo tena kwenye ule wakati wa kuwa na washambuliaji hatari wengi kwenye kikosi chao. Kuna wakati walihawahi kuwa na Donald Ngoma, wakawa na Amis Tambwe(ambaye alikuwa kwenye kiwango kikubwa), wakawa na Obrey Chirwa, pamoja na Simon Msuva aliyekuwa anatokea pembeni mwa uwanja na kufunga magoli mengi.

Sasa hivi hawana idadi kubwa ya hawa washambuliaji ambao ni hatari. Mrisho Ngassa Yuko kwenye siku zake za mwisho katika Mpira, hii ni kama ilivyo kwa Amis Tambwe.

Zahera, Kocha wa Yanga

Kwa hiyo Makambo ndiye mtu pekee ambaye anaangaliwa pale mbele kama kiongozi wa mashambulizi. Timu inamwangalia yeye tu. Kwa hiyo kipindi ambacho timu inataka goli, timu humtazama yeye kama mtu ambaye anaweza kuipa.

Huyu ndiye ambaye anatakiwa kuibeba timu kwa wakati, hasa hasa kwenye nyakati ngumu. Nyakati ambazo timu imebanwa na inahitaji njia mbadala ya kufunga goli ili iweze kupata alama tatu.

Nyakati hizo hutokea sana kama Jana ambavyo zilivyotokea kwenye mechi dhidi ya Ndanda FC.Mechi ambayo Yanga ilibanwa sana, mpaka ikalazimisha sare.

Mechi ambayo ilikuwa inamwihitaji mtu ambaye angeweza kuiweka timu kwenye mabega yake na kuibeba. Ndipo hapo macho ya wengi yalikuwa yanamwangilia Makambo.

Jaffaru Mohammed akishangilia

Hata alipokosa goli la wazi lawama zilienda kwake. Hata kocha wake Mkuu Mwinyi Zahera alionekana kutofurahishwa sana mpaka akamsema kwenye mkutano wa waandishi wa habari. Alifikia mpaka hatua ya kusema nafasi ile hata mama yake angeweza kufunga. Hii kauli ilikuwa siyo nzuri kulingana na mazingira ambayo aliyatolea. Huwezi jua mapokeo ya mchezaji atapokeaje?.

Kuambiwa kitu kama hiki kwenye mkutano wa waandishi wa habari ni kunaweza kumuumiza mchezaji, sawa, alikosa nafasi ya wazi kitu ambacho ni kawaida, kitu ambacho unaweza kukaa naye mazoezini na kumwambia ile ajirekebishe.

Mwinyi Zahera amekuwa akitoa kauli nyingi sana za kuwakosoa wachezaji wake. Kitu ambacho wakati mwingine ni kizuri lakini kuna aina ya ukosoaji. Unatakiwa kumkosoa mchezaji kwa kumjenga, na siyo ukosoaji wako uwe sehemu ya kumbomoa Mchezaji.

Sambaza....