Sambaza....

Tottenham Hotspurs katika mchezo huu walicheza mfumo wa 4-2-3-1 wakati Arsenal walicheza mifumo miwili ndani ya mchezo huu, mfumo wa kwanza ulikuwa 4-3-3 na mfumo wa 4-5-1 kwa nyakati tofauti.

Wakati walipokuwa wanashambulia Arsenal walikuwa wanacheza mfumo wa 4-3-3 na walipokuwa wanajilinda walikuwa wanatumia wa 4-5-1 ambapo Ozil na Mkhtaryian walikuwa wanashuka chini katikati kusaidia kukaba na kuongeza idadi ya watu katikati kuwa watano.

Mbele alikuwa anabaki mchezaji mmoja ambaye ni Pierre-Emirick Aubameyang, lengo kuu la Arsene Wenger lilikuwa kuiwezesha timu isitengeneze uwazi kati ya eneo la kujilinda ( eneo la beki) na eneo la katikati mwa uwanja. Na pia iwe rahisi kwao wao kuanzisha mashambulizi ya kushitukiza. Kipindi cha kwanza walifanikiwa kwa kiasi kidogo ambapo walijaribu kutengeneza mashambulizi mawili ya kushitukiza.

Kwanini hawakuwa na uwezo wa kutengeneza mashambulizi mengi ya kushitukiza?

Pamoja na kwamba Arsene Wenger alifanikiwa kutetengeneza uwazi kati ya safu ya ulinzi na safu ya kiungo lakini timu yake ilikuwa na uwazi kuanzia eneo la kiungo cha kushambulia na eneo la ushambuliaji , kuna wakati Aubameyang alionekana yuko peke yake bila msaada.

Hii ilisababishwa na nini ? Moja ni ubora wa kiungo cha kuzuia cha Tottenham Hotspurs kilichokuwa chini ya Eric Dier na Dembele ambao waliwalazimisha Arsenal watengeneze uwazi kati ya eneo la kiungo cha kushambulia na eneo la safu ya ushambuliaji.

Pili, Ozil na Mkhtaryian hawakuwa huru kumsaidia Aubameyang, mfano Mkhtaryian aliwekwa acheze upande wa kushoto, lengo la Arsene Wenger lilikuwa kumfanya Trippier awe na hofu ya kupanda mbele mara kwa mara kushambulia.

Lakini kumchezesha kushoto Mkhtaryian eneo hilo lilimnyima uhuru na kuonekana kutokuwa na msaada mkubwa kwenye timu.

Pia wakati Arsenal wanakaba walikuwa wanakaba nafasi na kukabia macho, hawakuwafanya Tottenham Hotspurs waonekane kama wanaharasika wakiwa na mpira, Tottenham Hotspurs wakati wakiwa na mpira walionekana huru bila kusumbuliwa na mtu, huku Arsenal wakiwa wamewekeza muda wao kukaba nafasi.

Kitu ambacho ƙkilikuwa na madhara kwao kwa sababu kiliwapa uhuru Tottenham Hotspurs kupanga mipango yao ya kushambulia bila kusumbuliwa ( wakiwa huru ). Mfano goli la kwanza wakati Davies anapata mpira alikuwa peke yake, hakukuwepo mtu wa kumsumbua na hii ilimpa uwezo mkubwa wa kutafakari kwa ufasaha ni eneo gani aupeleke ule mpira, na mipango yake ilitimia kwa sababu alimuona Kane akiwa peke yake katikati ya mabeki wawili ambao walikuwa wamempa uhuru Kane kuanzia alipokuwa anakimbia mpaka alipoenda kusimama eneo ambalo lilimwezesha kupiga mpira kwa kichwa hakukuwepo na mtu wa kumkaba au kumuharasi.

Hata baada ya kufunga goli kuna kichwa Kane alipiga kikatoka nje, wakati anakipiga alikuwa huru katikati ya mabeki wawili wa Arsenal.

Hii inaonesha mabeki wa kati wa Arsenal hawakuwa na uelewano mzuri kwenye kukaba, pia ukabaji wa timu kiujumla wa kukaba nafasi na kukabia macho ulikuwa unaigharimu timu.

Ukabaji huo uliwapa uhuru sana Tottenham Hotspurs, hii ilikuwa tofauti na kwa Arsenal wakati walipokuwa na mpira.

Tottenham Hotspurs walikuwa wanaanza kukabia juu, Son, Delle na Kane walikuwa wanakabia juu kipindi Arsenal ilipokuwa na mpira.

Hali ambayo iliwanyima Arsenal uhuru wa kuanzisha mashambulizi eneo la nyuma. Iliwalazimu wao kupoteza umiliki wa mpira kwa kupiga mipira mirefu mbele, na muda mwingi mabeki wake walikaa nyuma ya eneo lao na hawakuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi.

Hii ilikuwa tofauti na kwa mabeki wa Tottenham Hotspurs ambao walikuwa huru kusogea mpaka eneo la katikati mwa uwanja , walikuwa huru kuisaidia timu kujenga mashambulizi kwa sababu Pierre-Emirick Aubameyang alikuwa hakabii juu.

Tottenham Hotspurs waliwanyima nafasi ya kuwa huru Arsenal kila walipokuwa wanakaa na mpira kwa sababu kila Arsenal walipokuwa na mipira waliwaharasi na kuwanyima uhuru wa kupanga mipango yao.

Eric Dier alikuwa madhubuti kuwalinda mabeki wake kitu ambacho kilimpa ƴuhuru Dembele kuwa anapiga pasi kwa watu wa mbele kuanzia kwa kina Alli, Erricksen na Son.

Kuna wakati Alli, Erricksen na Son walishuka katikati ya uwanja kuongeza idadi ya watu eneo la katikati mwa uwanja hali ambayo ilitia ugumu kwa Arsenal.

Eneo la katikati mwa uwanja ndiyo lilikuwa eneo ambalo lilikuwa silaha kwa Tottenham Hotspurs.

Kwa hiyo Tottenham Hotspurs kushinda mechi ya jana ya North london Derby kumewafanya wapate alama 7 dhidi ya timu tatu kubwa katika mechi za hivi karibuni, wakitoka sare na Liverpool, na kuwafunga Arsenal na Manchester United na kuwafanya waende michezo 13 bila kufungwa katika uwanja wao wa nyumbani na katika michezo hiyo 13 wakifanikiwa kufunga magoli 33, na mara ya mwisho kwao kufungwa ilikuwa kwenye mechi dhdi ya Manchester City kwenye uwanja wa Etihad, tangu hapo wameenda michezo 9 bila kufungwa huku wakipata clean sheets 5 kwenye hiyo michezo 9 na kufunga magoli 21.

Kwa takwimu hizi Tottenham hotspurs wanatakiwa wajitazame upya namna ya wao kufanya wawe timu ya kushinda makombe na siyo timu ya kutoa ushindani

Sambaza....