Jana kulikuwa na mechi ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa, Yanga dhidi ya KMC. Mechi hii ilikumbwa na tukio moja ambalo limezua mjadala mkubwa.
Tukio la Ally Ally kujifunga kwa kichwa akiwa kwenye harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Ibrahim Ajib. Kiufundi kipi kilisababisha Ally Ally kujifunga ?
Kutokuwepo katika eneo lake sahihi.
Kabla ya mpira kupigwa, Ally Ally alikuwa katika eneo ambalo halikuwa eneo sahihi kwake yeye kutakiwa kuwepo, ndiyo maana mpira ulipokuja hakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi mazuri ya kuuokoa ule mpira kwa sababu tu ya eneo ambalo alikuwepo awali.
Makambo anastahili pongezi.
Eneo ambalo alikuwa amejiweka lilikuwa eneo ambalo lilimlazimisha Ally Ally kufanya makosa. Kwanini ?, Makambo alikuwa anakimbia nyuma ya beki.
Mshambuliaji anapokuwa anakimbia nyuma ya beki, kuna madhara hasi kwa beki huwa yanatokea. Kwanza , beki anakuwa anakimbia huku akitazama uelekeo wa mpira utakaopigwa na mchezaji wa timu pinzani.
Pili, beki pia atakuwa anakimbia huku akimtazama mshambuliaji aliyepo nyuma yake. Kwa hiyo hapo itamlazimu afanye vitu hivo viwili, kukimbia huku anatazama mpira na pia kukimbia huku anamtazama mshambuliaji wa timu pinzani.
Ndicho kilichofanyika, Ally Ally alikuwa anakimbia huku anamtazama Ajib ambaye alikuwa anapiga krosi, pia alikuwa anakimbia huku anamtazama Makambo aliyekuwa nyuma yake.
Kiasi kwamba wakati mpira unafika eneo lake alilazimika kufanya maamuzi ya kuuokoa huku akijua kuwa kama atashindwa kuokoa mpira ule basi Makambo ambaye alikuwa nyuma yake alikuwa na nafasi ya kufunga, hivo Makambo alimlazimisha Ally Ally kufanya makosa.