Sambaza....

ACHANA na kukosa mdhamini, sahau kuhusu mechi kumi mfululizo za Yanga SC katika uwanja wa Taifa, sahau kuhusu timu moja kuwa mbele michezo mitatu hadi minne katika –siku ya sita tu ya msimu, je, unafahamu kuwa michezo ya leo Jumatano kati ya Ruvu Shooting vs African Lyon, Singida United vs Mbeya City FC inakamilisha siku saba mfululizo za Mungu ligi kuu Tanzania Bara ikichezwa?!

Hii ni ligi kuu ya kwanza duniani kuchezwa kwa siku saba mfululizo, mechi ya Stand United vs Tanzania Prisons kesho Alhamis itakuwa ni siku ya nane mfululizo, Azam FC watacheza Ijumaa na kukamilisha siku ya tisa mfululizo ligi ikichezwa, Jumamosi itakuwa siku ya kumi mfululizo na mchezo wa Dar es Salaam-Pacha, Simba SC vs Yanga SC Jumapili hii utafanya ligi hii kuchwa kwa siku 11 mfululizo!

Ni maajabu makubwa, je, ni uwanja mmoja tu unaotumika hadi kupelekea ligi kuu kuchezwa kwa mtindo wa michuano ya ‘Ndondo’? lakini hata huko katika michuano ya mtaani zipo siku ambazo huwapumzisha mashabiki.

Kucheza mdfululizo kila siku ya Mungu kunaondoa utamu wa ushindani, je, Wallace Karia ambaye aliingia madarakani yapata mwaka mmoja uliopita kama rais wa TFF aliongeza idadi ya timu-kutoka 16 hadi 20 ili kuua kabisa mpira wa Tanzania uliokuwa ‘ICU’? ametuletea ligi kuu ya wapi inayochezwa kila siku hadi kwa siku 11 mfululizo?

Amepelekea ligi kukosa udhamini kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1997, na kwa mara ya kwanza katika historia Shirikisho la soka linatangaza hadharani kuwa michezo ya Yanga na Simba ambayo ilipangwa katika ratiba kuchezwa katikati ya wiki hii inaahirishwa ili kuzipa nafasi ya kujiandaa klabu hizo kubwa nchini kuelekea mchezo wao wa Jumapili hii. Hii ni ligi kuu ya wapi?

Sambaza....