Wakati wa uongozi wa Jamal Malinzi, alianzisha programu moja ambayo ilibezwa sana. Bila kuangalia mambo mengine yaliyohusishwa na hii programu iliyopewa jina la MABORESHO, ilikuwa ni muhimili mkubwa sana wa kuzalisha wachezaji kwa mtazamo wao. Ingawa moja ya swali kuu lilikuwa wachezaji hao iweje wacheze moja kwa moja timu ya Taifa? wakati kuna wachezaji wengi tu waliokuwa wakicheza ligi kuu. Maboresho ilikuwa sera yao, na Rais wa sasa akiwa moja ya watekeleza sera hiyo. Wachezaji waliwekwa katika kambi huko Tukuyu wakifanya mazoezi na kufundishwa uzalendo kwa kuimba wimbo wa taifa kila asubuhi.
Mwaka 2016 TFF iliibuka na wazo la kuwatunza U13 kupitia kituo cha Alliance pale Mwanza ambacho kiliwazaa kina Kelvin John. Kituo ambacho kwa kiwango fulani kinasaidia pia.
-Maboresho wakiwa kambini
Shirikisho la soka la Tanzania, TFF, awamu hii limedhamilia kwa dhati kabisa kutekeleza programu ya soka la vijana. Tanzania kwa mara ya kwanza kuliko kipindi chote imefanikiwa kuzifanya timu za taifa madaraja yote kushiriki michuano mikubwa. Achilia mbali matokeo mazuri (Tanzanite kushinda COSAFA) na Mabaya (Serengeti Boys kuishia vibaya hatua ya makundi tulipokuwa wenyeji bila alama na Taifa stars kushindwa kupata hata alama moja AFCON 2018).
Soka la vijana ni muhimili muhimu sana kwa sasa ya baadae. Unakumbuka enzi za Iddi Kipingu? enzi za Makongo alivyoweza kuwatunza na kuwaibua wachezaji kama Juma Kaseja. Aliweza kuwaweka shuleni huku wakicheza mpira wa miguu. Ni matokeo ambayo tunamaanisha hapa kwa mustakabali wa soka letu.
-Juma Kaseja
TFF wana ligi mbalimbali za vijana na mashindano mbalimbali, lakinu hawa watoto wanaishia wapi baada ya michuano?
‘Kikao cha TFF na Fountain Academy kilikuwa muhimu, lakini pia mkutani na waziri ulikuwa muhiku’- Taarifa ya TFF wakati wakijitetea kwanini hawakuweza kuhudhuria kikao kikichoitishwa na Mh Mwakyembe, Waziri mwenye dhamana na michezo nchini.
-TFF na Fountain Fate Academy wakitia saini
Mwezi Julai mwaka huu TFF waliingia makubaliano na shule nzuri kabisa ya Fountain Gate Academy ya Jijini Dodoma. Lengo kuu la makubaliano haya ni swala zima la namna gani ya kuwahifadhi vijana wanaofanya vizuri katika michuano ya shirikisho na kufanya urahisi wa kuwapata pindi wanapohitajika.
‘Hapo mwanzo ilikuwa tabu kuwatafuta tena vijana baada ya mashindano kumalizika, na pia kuwafuatilia maaendeleo yao’ Ofisa mmoja aliimbia Kandanda. ‘Lakini sasa, vijana hao wanaendwlea kupata elimu huju wakipata na mafunzo ya mpira katika shule hii yenye hadhi yake’ alioongeza.
Katika makubaliano kati ya TFF na Fountain Gate Academy ni kuwa kutakuwa na ushirikiano kuwatunza Wachezaji wa Timu za Taifa U13,U15 na U17 katika Shule ya Fountain Gate huku wakiendelea kupatiwa elimu na mafunzo ya Soka kwa kipindi chote.
“Wachezaji wote waliopatikana baada ya ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 15 kumalizika na kuchaguliwa na jopo la makocha mbalimbali watachukuliwa na kulelewa kwenye shule hiyo iliyopo jijini Dodoma na kupatiwa mahitaji yote ya kawaida na hata yale ya kimichezo zaidi,” alisema Ndimbo, Afisa Habari wa TFF, wakati wa kutagaza uamuzi huo.
Baada ya muda kidogo tunaenda kuwatengeneza kina Yusuf Mlipili, Joram Mgeveke, Benedict Tinoco, Said Juma Makapu wa maboresho au Juma Kaseja, Jerry Tegete, Juma Abdul kutoka Makongo kutoka katika huu utararibu wa Fountain Academy.
Huu ndio inabidi uwe utaratibu endelevu, ikiwezekana hata makampuni binafsi yawekeze hivi au shule za michezo ziwe zinasajili wachezaji hawa ili zije zifanye biashara hapo mbeleni kwa manufaa ya nchi na wao wenyewe. Wachezaji hawa pia wapewe vitambulisho maalumu vyenye namba peke ya utambulisho wa kisoka, ambayo inatunza kumbukumbu za mchezaji husika kila aendako. Vitambulisho hivi vinaweza pia kugaiwa kwa wachezaji wote wenye leseni ya kucheza nchini kwa utaratibu maalumu.