Klabu ya soka ya Manchester United ipo mbioni kuwaachia nyota wake sita katika kipindi cha majira ya joto kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuisha mikataba, kupungua viwango vyao pamoja na sababu nyingine mbalimbali.
Nia hiyo ni maalumu kwa ajili ya kumsaidia Kocha Ole Gunnar Solskajaer kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho ambacho msimu ujao kinataka kuwepo kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu England.
Hata hivyo mipango hiyo ambayo inawahusisha nyota wengine wenye majina makubwa huenda ikaathiriwa na wachezaji kama Ander Herrea, Juan Mata na Alexis Sanchez ambao pengine kuondoka kwao kunaweza kukaiathiri klabu hiyo.
Taarifa za ndani zinasema Ole amepanga kumuachia mshambuliaji Sanchez kuondoka lakini mshahara wake unafanya mpango huo kuwa mgumu zaidi, lakini pia wachezaji kama Herrera na Mata ambao bado Ole anawahitaji huenda wakaruhusiwa kuondoka baada ya kudai kulipwa mshahara mkubwa wakati ambapo mikataba yao ikiwa ukingoni.
Mpaka sasa hakuna uhakika kama makubaliano ya kuwaongezea mikataba nyota hao itafikiwa ukizingatia kuwa umri wao umekwenda huku wakihitaji kulipwa pesa nyingi ili kukubali kusaini mkataba mpya na Manchester United, huku kwa Herrera tayari akitajwa kuwa ameshafanya makubaliano ya awali na Paris Saint Germain ili kujiunga nao mwezi wa saba.
Kwa upande wa Sanchez ambaye alisajiliwa mwaka jana na Jose Mourihno akitokea Arsenal, mshahara mkubwa anaolipwa pamoja na baadhi ya vipengele vya mkataba vinamfanya kocha Ole ambaye amemtumia mara 11 tu toka awe kocha wa klabu hiyo kuumiza kichwa namna ya kumuondoa klabuni hapo.
Mwaka jana jarida la Der Spiegel liliandika kwamba Sanchez analipwa Paundi 391,000 kwa juma huku akiongezewa Paundi 75,000 kwa kila mchezo anaoanza, jambo linazifanya hata zile klabu tano kubwa barani Ulaya kusita kutangaza dau la kumnyakua mshambuliaji huyo ambaye hajaonesha cheche zozote akiwa na Manchester United.
Mchezaji mwingine ambaye anaweza kuondoka majira ya Joto na Paul Pogba ambaye naye licha ya kuwepo taarifa za kuondoka klabuni hapo toka enzi za Jose Mourihno ameibua mjadala mwingine wakati wa mapumziko ya mechi za Kimataifa akisema ana ndoto za kucheza Real Madrid iliyochini ya kocha Zinedine Zidane.
Kauli ya Pogba imeongeza shaka katika kambi ya Manchester United jambo ambalo linazidi kumuumzia kichwa Ole iwapo amruhusu kiungo huyo kuondoka msimu huu ama kusubiri hadi msimu ujao, japokuwa wachezaji waliopita kwenye klabu hiyo wakishauri Pogba aachwe aondoke mwishoni mwa msimu huu kwani amekuwa kama kirusi ndani ya timu hiyo.
Nyota mwingine ambaye tayari ameshaanza kukunja nguo zake na kuzitia kwenye begi ni Antonio Valencia beki wa pembeni ambaye ameshaanza mipango ya kujiunga na klabu moja huko nje Marekani.
Mkataba wa Valencia unaisha mwishoni mwa msimu huu na hakukuwa na maongezi yoyote ya kuongeza mkataba kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye alijiunga na miamba hiyo ya soka mwaka 2009 akitokea Wigan.
Mpaka sasa licha ya tetesi za chinichini Ole ana uhakika wa kumbakisha Mlinda Mlango nambari moja David de Gea kwa msimu ujao ambaye naye ameonesha nia ya kubaki klabu hapo na kukubali kusaini mkataba mpya.