Sambaza....

Wananchi Yanga wamefuzu kwa mara ya kwanza kwenda robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika  baada ya kushindwa kufanya hivyo mara mbili iliposhiriki hatua ya makundi mwaka 2016 na 2018.

Yanga si tu imefuzu lakini pia imeongoza kundi D lililokua na Real Bamako, TP Mazembe na US Monastir waliomaliza katika nafasi ya pili. Na faida watakayoipata Yanga ni kuanzia ugenini katika mchezo wa robo fainali. 

 

Timu nyingine zilizofuzu ni Marumo Gallants, USM Algier, Pyramids, AS FAR, Rivers United. Yanga atakwenda kukutana na mshindi wa pili kutoka Kundi A,B au C ambao ni Rivers United (Nigeria), USM Algier (Algeria) na Pyramids ya Misri. Tuzitazame kwa undani timu hizi tatu ambazo moja kati yao itakutana na Yanga robo fainali.

USM Algier

Wamefuzu kutokea kundi A nyuma ya Gallants wakiwa na alama 11 wakifunga mabao 11 na wakiruhusu mabao 5. Wamefungwa mchezo mmoja pekee katika kundi lao na mingine yote wakishinda na kutoka sare.

Katika Ligi yao nchini Algeria hawapo katika kiwango kizuri kwani wanashika nafasi ya sita wakiwa na 29 katika michezo 17 waliyocheza. Anaeongoza Ligi ni CD Belouzdaid mwenye alama 40. 

Klabu hiyo ni kongwe kama Yanga kwani nayo imeanzishwa mwaka 1935 na uwanja wanaoitumia katika mechi zao za nyumbani ni Omar Hamad. 

USM Algier.

Rivers United.

Wanaijeria hawa wamefuzu kutoka kundi B na vigogo wenzao kutoka Afrika Magharibi wakiwa na alama 10, wakifunga mabao tisa na kuruhusu mabao saba. 

Katika Ligi kuu nchini kwao Rivers wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama 19 nyuma ya vinara Lobby Stars wenye alama 20. Hata hivyo Rivers wana viporo viwilo hivyo huenda warudi vyema na kuongoza Ligi. 

Endapo Yanga watapangwa na Rivers ni wazi itakua ni wakati sahihi kwa wao kulipa kisasi kwani katika msimu uliopita Wananchi walipigwa nje ndani ya Wanaija hao katika micheza ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Rivers United

Pyramids Fc

Mafarao hawa hawakua na wakati mzuri msimu huu kwani iliwapasa kusubiri mpaka mchezo wa mwisho dhidi ya ndugu zao Future Fc walipopata ushindi na kujihakikishia kuvuka kwenda robo fainali. Wamemaliza nyuma ya AF FAR wakiwa sawa kwa alama 11 wakitofautishwa kwa tofauti ya bao moja pekee.

Pyramids kama ilivyo ada katika Ligi bado wameshindwa kuweka utawala wao mbele ya Al Ahly na wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 39, huku Ahly akiwa kinara kwa alama 44. 

Pyramids Fc

Matajiri hao wa Misri wanatumia uwanja wa 30 June wanawajua vizuri Yanga kwani tayari walishakuka nchini kucheza na Wananchi na walifanikiwa kuwaondosha Yanga katika Playoffs ya Kombe la Shirikisho. Katika mchezo ambao Yanga walichezea mkoani Mwanza Mafarao hao iliwapasa kuja nchini na ndege yao binafsi ili kurahisisha safari yao.

Ni wazi sasa Yanga watapata kujiuliza kwa mara nyingine tena mbele ya Wamisri hao endapo watapangwa kukutana tena katika droo itakayofanyika leo nchini Misri majira ya saa tatu na nusu usiku.

Sambaza....