Sambaza....

Kama wewe ni mfuatiliaji wa soka barani ulaya bila shaka, utakuwa unaijua Barcelona, klabu kubwa na yenye mafanikio makubwa barani ulaya na duniani kwa ujumla.

Jana Barcelona ilikuwa uwanjani kukwaana na kikosi cha Maurizio Pocchetino, Tottenham, na kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa mwisho katika hatua ya makundi klabu bingwa barani ulaya.

Katika mchezo huo Barcelona wakiwa nyumbani,Camp nou  waliingia wakiwa hawana presha kwani tayari walikwisha fuzu raundi ya 16 boraya mashindano hayo, na kumfanya kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde kufanyamabadiliko katika kikosi chake kilichoanza katika mchezo huo.

Wote tunajua kuwa aina ya soka wanalocheza miamba hiyo ya Hispania, Barcelona  ni kumiliki mpira na kushambulia kwa pasi fupi na ndefu ,kwa kiasi kikubwa hupenda kukaa na mpira muda mrefu na kutengeneza nafasi za kufunga.

Mwaka 2006 katika michuano kama hii ya klabu bingwa barani ulaya, Barcelona ilizidiwa kiasi cha umiliki wa mpira na kufikia asilimia 42 pekee dhidi ya Werder Bremen katika hatua ya makundi, kuanzia mwaka huo, Barcelona hawajawahi kuzidiwa umiliki hadi jana katika mchezo wake dhidi ya Tottenham.

Barcelona walimiliki mpira kwa asilimia 48 pekee wakizidiwa na Tottenham waliomilkiki kwa asilimia 52 na kuvunja  falsafa ya timu hiyo ya kumiliki mpira.

Sio tu kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya hata kwenye ligi ya Hispania, Barcelona wamekuwa na falsafa hiyo ya kumiliki mpira katika vipindi vyote viwili. Katika mechi za hivi karibuni dhidi ya Alaves na Valencia , Barcelona walimiliki mpira kwa asilimia 78 na 76 mtawalia ikiwa ni wastani wa asilimia 77.

Sare hiyo ya 1-1 hatimaye Tottenham imefuzu katika hatua ya 16 bora ya klabu bingwa ulaya. Tottenham ambao walijikusanyia alama 1 katika michezo mitatu kati ya sita ya michuano hiyo wamejikuta wakimshukuru Christian Eriksen kwa goli aliloifungia Tottenham dhidi ya Inter Milan, pale San Siro, katika kichapo cha magoli 2-1.

Sheria za shirikisho la soka barani ulaya zimewabeba Tottenham kwani, Tottenham na Inter Millan wote wamejikusanyia alama 7, na uwiano sawa wa magoli, kilichotazamwa baada ya hayo yote kuwa sawa ni tofauti ya magoli kwenye mechi zilizokutana klabu hizo, wote wakiwa na magoli 2, lakini Tottenham imefuzu kutokana na faida ya goli la ugenini  dhidi ya Milan.

Sambaza....