KATIKA umri wa miaka 31 kiungo mshambulizi na mshindi mara nne wa ligi kuu Tanzania Bara, Haruna Moshi Shaaban ´ Boban´ ameingia katika kikosi cha wakali waliowahi kuzichezea klabu hasimu nchini Yanga SC na Simba SC.
Boban ambaye alichezea Coastal Union ya Tanga kwa muda mfupi wakati akiwa kinda mwaka 2000, Moro United 2000, Simba 2003-2009, Gelfe ya Sweden kwa muda mfupi pia msimu wa 2009/10, Simba 2010-2013.
Kwa misimu minne tangu alipomaliza mkataba wake Simba Juni 2013 amekuwa ´akitangatanga´ katika klabu za Coastal, Friends Rangers, Mbeya City FC Alhamis hii amekamilisha usajili wa kujiunga na wababe wa soka la Tanzania, Yanga akitokea African Lyon aliyoijiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu.
NI KAMARI…
Kocha wa viongozi hao wa ligi kuu, Mcongoman, Zahera Mwinyi tayari amesema hadharani kwamba usajili huu ni mapendekezo yake. Zahera amekuwa nchini kwa nusu mwaka tu lakini ´macho yake makali´ yameweza kuona kipaji hiki ambacho hakihitaji utambulisho kwa wapenzi wa soka nchini.
Kwa Boban, Zahera amepata silaha ambayo itaongeza utulivu katika eneo la mashambulizi. Si hivyo tu, Haruna ni mchezesha timu mwenye jicho la tatu katika upigaji wa pasi za mwisho, na ni mfungaji mzuri mwenye uwezo wa kufanya hivyo akitokea upande wowote ule wa uwanja.
Licha ya usajili huu kukamilika bado kumekuwa na wasiwasi mkubwa kwa mashabiki na wanachama wa mabingwa hao mara 27 wa kihistoria nchini. Wasiwasi wenyewe si kutokana na uwezo wake uwanjani bali aina ya maisha ambayo mchezesha timu huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania amekuwa akiripotiwa.
Wiki iliyopita akiwa mchezaji wa Lyon, Boban aligoma kuambatana na timu hiyo huko mkoani Mbeya kwamchezo wa ligi kuu dhidi ya timu yake ya zamani, Mbeya City FC. Aligoma kwa madai ya kutolipwa stahiki zake (pesa ya usajili na mishahara yake ya miezi kadhaa.)
Msimu wake wa mwisho klabuni Simba aliondolewa kikosini na Kocha Mfaransa, Patrick Liewig na hakushiriki katika michezo tisa ya mwisho kati ya Februari hadi Mei 2013 na sababu kubwa Ilikuwa ni maslai.
Kocha Liewig alimuondoa kikosini Boss na kundi la mastaa kama Mzambia, Felix Sunzu, Juma Nyosso, Amir Maftah, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Chombo ´Redondo´ na licha ya kusemwa nidhamu yao ilikuwa sababu lakini ukweli wachezaji hao waligoma kwasababu hawakuwa wamelipwa mishahara yao kati ya November 2012 hadi Februari 2013.
Alipojiunga Coastal msimu wa 2013/14, Haruna hakumaliza msimu akajiondoa katika timu hiyo kwasababu zilezile za kimaslai. Misimu miwili iliyopita alisajiliwa City lakini mwanzoni mwa mwaka 2016 akajiondoa katika klabu hiyo ya Mbeya kwa mara nyingine sababu za kimaslai zilitajwa.
Kila anapojiondoa katika klabu ya ligi kuu, Boban amekuwa kijana mtiifu katika timu ya darajala kwanza Friends Rangers na msimu uliopita alijaribu kadri alivyoweza kuisaidia timu hiyo kupanda ligi kuu.
Swali la kujiuliza ni kwanini Haruna hucheza bila matatizo akiwa Rangers timu ambayo haina chochote? Kwa mtazamo wangu, ni HEKIMA. Boban ukimuheshimu hata kama huna chochote atakufanyia kazi nzuri. Haruna hapendi kudharauliwa, kudanganywa danganywa kama mtoto mdogo na hupenda utulivu.
Nimefurahi kukamilika kwa usajili wake klabuni Yanga na wakati huu migomo ya wachezaji ikiwa mara kwa mara katika timu hiyo kutokana na wachezaji kudai stahiki zao, kocha Zahera anapaswa kuelewa licha ya kipaji kikubwa cha Boban ndani ya uwanja usajili alioufanya ni ´kamari´ ambayo yeye mwenye anaweza kuicheza.
Kama kamari hii itakuwa bora kwa hakika Boban ni kipaji kitakachochangia taji la 28 la ligi kwa ´Timu ya Wananchi´ msimu huu. Huyu ni namba kumi atakaye wasahulisha watu kuhusu uvivu wa Ibrahim Ajib. Lakini inaweza kuwa kamari mbaya kwa Zahera kama Haruna hataheshiwa na kupewa stahiki zake.
Kuwa na Boban, Mrisho Ngassa, Kelvin Yondan,Thaban Kamusoko, Amis Tambwe, Deus Kasekeni faida kubwa kwa Zahera. Kazi kwake.