Kocha wa Napoli Carlo Ancelotti amesema hali ya mlinda mlango wa timu hiyo David Ospina aliyepoteza fahamu jana kwenye mchezo wa ligi ya Italia (Seria A) kati yao na Udinese inaendelea vizuri na hakuna jambo kubwa sana la kiafya.
Ancelotti amesema wanashukuru baada ya vipimo imeonesha kuwa Ospina hana tatizo kubwa kama ambavyo walidhani kutokana na namna alivyoshindwa kuendelea na mchezo hapo jana.
“Ni kama bahati nzuri kwetu, hakuna jambo kubwa sana, amerejewa na fahamu, walifanya vipimo vya CAT Scan na kugundua halikuwa tatizo kubwa,” amesema.
Ospina alidondoka jana wakati timu yake ikipepetana na Udinese kwenye mchezo ambao walishinda kwa mabao 4-2.
Awali kwenye mchezo huo Ospina ambaye anachezea Napoli kwa mkopo wa muda mrefu akitoka Arsenal aligongana na beki Ignacio Pussetto lakini aliendelea na mchezo lakini baada ya kufungwa bao la pili hali yake ilibadilika na ikabidi atolewa mapema na kukimbizwa hospitalini.
Ospina mwenye umri wa miaka 30 alijiunga na Napoli mwaka jana mwezi Agosti na kabla ya hapo aliichezea Arsenal michezo 27 tu ya ligi toka ajiunge nayo mwaka 2014