Kiungo wa majogoo wa jiji Liverpool Naby Keita, amesema anaendelea vizuri, baada ya kufikishwa hospitali usiku wa kuamkia jana, kufuatia majeraha ya mgongo alioyapata akiwa katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya SSC Napoli.
Mchezo huo uliomalizika kwa Liverpool kufungwa bao moja kwa sifuri, ulishuhudia kiungo huyo kutoka nchini Guinea, akipata majeraha hayo dakika ya 19, na baadae kukimbizwa hospitali ya mjini Naples kwa matibabu zaidi.
Mapema jana Kaita alithibitisha kuendelea vizuri, na anaamini matibabu aliyopatiwa tangu alipofika katika hospitali ya mjini Naples-Italia, yamemsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida, japo atahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa madaktari wa klabu ya Liverpool.
Kabla ya mchezaji huyo kuthibitisha anaendelea vyema, daktari mkuu wa klabu ya Liverpool alionyesha kuwa na wasiwasi na hali ya Keita, huku akiwataka waandishi wa habari kuwa na subra.
“Keita anapatiwa matibabu, tutawapa taarifa zaidi baadae, kwa sasa hatuwezi kusema lolote kwa sababu hakuna anaejua nini kilichomsibu, zaidi ya kusubiri majibu ya vipimo alivyofanyiwa.” Alisema daktari, mara baada ya mchezo dhidi ya SSC Napoli.
Leo mchana Keita alitarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitali na kuanza safari ya kurejea jijini Liverpool-England.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna taarifa zinazoeleza kama kiungo huyo ataweza kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza dhidi ya Manchester City katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England, mwishoni mwa juma hili.
Keita, alisajiliwa na Liverpool akitokea RB Leipzig kwa ada ya Pauni milioni 48, mwishoni mwa msimu uliopita, na mpaka sasa ameshacheza michezo tisa ya ligi ya England, huku akianzishwa kwenye kikosi cha kwanza mara nne.