Hizi ni habari mbaya, si nzuri hata kidogo kwa mashabiki na klabu ya Liverpool kwa ujumla, hii ni baada ya kinara wa ufungaji katika klabu hiyo Mohamed Salah kuzawadiwa mkwaju wa penati baada ya kumdanganya muamuzi katika mchezo wa ligi uliochezwa jana dhidi ya New Castle United ya Rafa Benetiz.
Lilikuwa ni goli la pili ambapo, Mo Salah alivutwa kidogo mkono wake wa kushoto na beki wa New Castle, Paul Dummett katika kipindi cha pili na mwamuzi wa mchezo huo Graham Scott kutenga tuta. Penati hiyo ambayo ilitiwa kimywani na Salah imezua utata, na kudai kuwa Salah alijiangusha ili kumlaghai mwamuzi na kwa kesi kama hizi kitakachotokea ni kufungiwa mechi mbili baada ya kamati ya mashindano kulijadili suala lake.
Kama Salah atafungiwa mechi mbili, basi atazikosa mechi dhidi ya Arsenal tarehe 29 mwezi huu na ile dhidi ya Man City, tarehe 3 mwakani.
Liverpool kwa mara ya kwanza imezawadiwa penati katika uwanja wa nyumbani tangu octoba 28, mwaka 2017. Mashabiki waliohudhuria mtanange huo walishangaa kuona Liverpool ikipewa penati nyepesi kiasi kile.
Baada ya mchezo, kocha wa New Castle, Rafa Benetiz amedai kuwa, goli la pili ambalo ni la penati liliwanyong’onyesha wachezaji wake kiasi cha kuruhusu magoli mengine mawili.
“Isingekuwa mwamuzi kutoa penati nyepesi, tusingezungumza haya sasaivi, vijana wangu walikatishwa tamaa na mwamuzi baada ya goli la pili”.
Kikubwa kunachosubiliwa ni maamuzi ya kamati ya mashindano ya FA, kama Salah atakutwa na hatia ya kumdanganya muamuzi kwa kujiangusha atazikosa mechi mbili.
Mark Halsey, ambaye ni mwamuzi wa zamani wa ligi kuu Uingereza ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa, alichokifanya Salah hata bingwa wa kujiangusha Harry Kane hawezi kufanya hivyo.
“Kwa maoni yangu, lazima vitendo hivi vya uongo vidhibitiwe naona ni bora Salah akafungiwa mechi mbili ili kukomesha huu ugonjwa katika ligi yetu.”
Baada ya michezo ya jana Liverpool imekaa kileleni ikijikusanyia alama 51 katika michezo 19 iliyocheza, ikiwa na tofauti ya alama 6 dhidi ya Man City yenye alama 45 katika nafasi ya pili.
Hadi sasa Mo Salah ameifungia timu yake mabao 12,
akijaribu kutetea tuzo yake ya mfungaji bora wa ligi msimu uliopita kwa kufunga
magoli 32. Kwa sasa, anashika nafasi ya pili, akiwa sawa na Harry Kane wa
Tottenham Hotspurs chini ya kinara Pierre –Emerick Aubameyang wa Arsenal na
magoli yake 13, wengine ni Edin Hazard wa Chelsea mwenye magoli 10 katika
nafasi ya nne.