Kikosi cha Yanga tayari kimetua Jijini Mwanza baada ya kumaliza wiki ya maandalizi mkoani Shinyanga walipoenda baada ya kumaliza mchezi wao wa Ligi dhidi ya Biashara United.
Yanga walikwenda kujificha Shinyanga wakijiandaa na mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Simba utakaopigwa May 28 Jumamosi hii katika dimba la CCM Kirumba.
Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Geita Gold katika mchezo wa robo fainali. Awali walizitoa timu za Mbao, Biashara na Ihefu katika hatua za awali.
Kikosi cha Yanga kipo kambini kamili gado tayari kabisa kumvaa Mnyama katika mchezo wa kisasi kwa upande wao kwani msimu uliopita katika michuano hiyo walifungwa fainali mkoani Kigoma na Simba.
Ukiachana na Saidoo Ntibazonkiza na Dickson Ambundo wachezaji wengine wote walifanya mazoezi mkoani Shinyanga kwa mara ya mwisho. Hata majeruhi wa muda mrefu Yacouba Sogne alijumuika na wenzake katika mazoezi hayo.
Saidoo na Ambundo walifukuzwa kambini baada ya mchezo dhidi ya Baishara kutokana na matatizo ya kinidhamu.
Yanga wanategemea kua na kikosi kamili baada ya kuwapumzisha baadhi ya nyota wake dhidi ya Biashara ili kuepukana na majeruhi kuelekea mchezo huo muhimu. Nyota kama Feisal, Aucho na Diara hawakua sehemu ya kikosi kilichoanza mchezo wa mwisho dhidi ya Biashara Utd.
Ni wazi mwalimu Nabi atakua na kikosi kamili katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba ambayo imetoa suluhu michezo miwili mfululizo ya Ligi katika msimu huu.
Ni CCM Kirumba Mwanza ndio itakayoamua kama Wananchi watatetema au wataendeleza vilio katika kombe la FA.