DONALD Dombo Ngoma alifunga goli pekee na kuipa ushindi muhimu timu yake ya Azam FC katika mchezo wa ugenini dhidi ya Singida United jana Jumapili lakini kikubwa nilichokiona katika mchezo huo ni ubovu wa eneo la kuchezea ´pitch´ ya uwanja wa Namfua.
Uwanja huo ambao ulifanyiwa matengenezo makubwa mara baada ya Singida United kupanda ligi kuu mwaka uliopita haufai kwa usalama wa wachezaji kutokana na kutokuwa na nyasi sehemu nyingi.
Kwa namna ulivyo hivi sasa, tatizo kubwa linalochangia vipara hivyo ni maji na inaonekana wahusika hawaumwagili uwanja huo hata kidogo. Ni uwanja mgumu kutokana na kukosekana na huduma ya maji.
Si, Namfua tu, Alhamis iliyopita nilitazama pia mchezo kati ya Mbeya City FC na Mwadui FC katika uwanja wa Sokoine Mbeya. Huko nako kuna tatizo kubwa la ukosefu wa nyasi katika eneo la kuchezea. Sokoine Stadium nao umekuwa mgumu, hauna nyasi na sababu ni ileile tu- ukosefu wa mtunza uwanja.
Jamhuri Stadium, Morogoro, Mkwakwani Stadium, Tanga, Mabatini, Mlandizi, Karume Stadium, Musoma, Kambarage Stadium, Shinyanga navyo viko hovyo kabisa katika eneo la kuchezea na Nadhani TFF inapaswa kuvitazama viwanja hivyo kwa macho makali na kuvitoa kasoro.
TFF imesisitiza mara nyingi kuhusu suala la viwanja tutajaribu kupata ufafanuzi zaidi pia.
Ubovu huo wa pitch wakati mwingine unapunguza ufanisi wa wachezaji kwa mfano, Habib Kyombo kwa sababu za kiuwanja alishindwa kuisawazishia timu yake ya Singida United siku ya jana kutokana na mpira kuhamishwa na ubovu wa uwanja wakati akijiandaa kushuti akiwa karibu na kipa wa Azam FC, Razaq Abarola.
TFF na wahusika wa viwanja hivyo wanatakiwa kukaa chini na kutazama namna ya kufanya wakati ligi ikiendelea. shida kubwa ni utunzaji hasa umwagiliaji.