Msimu jana alishirikiana na kina Shiza Kichuya, Mzamiru Yasin kuibeba Simba.
Pamoja na uzito wa Simba , ugumu wa njia walizokuwa wanapitia lakini walifanya kadri wanavyoweza kuibeba Simba.
Simba ambayo ilikuwa bingwa wa kombe la chama cha soka nchini (TFF)
Simba ambayo ilishika nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Tanzania bara nyuma ya Yanga kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Simba ilikuwa haina safu kali ya ushambuliaji kitu ambacho kilichangia kwa namna moja au nyingine kuzidiwa na Yanga.
Simba iliwatumia kina Mohammed Ibrahim, Shiza Kichuya na wengine katika safu ya kiungo mshambuliaji ili kuhakikisha wanapata magoli.
Kiasi kwamba wachezaji hawa walifanikiwa kushika mioyo ya mashabiki.
Ilikuwa furaha kwa mashabiki kumuona Mohammed Ibrahim akiwa kwenye orodha ya wachezaji watakaoanza kwenye mechi husika kwa sababu walijua kuna vitu vingi watapata kutoka kwake.
Iwe anatokea pembeni mwa uwanja kulia au kushoto, awe anacheza nyuma ya mshambuliaji yani ”Inside ten” alikua na uwezo mzuri wa kuifanya Simba icheze vizuri kwenye utamaduni wake wa pasi nyingi na kushambulia kwa uelewano mkubwa.
Uwezo wake wa kumiliki mpira bila kupoteza, kupiga pasi sahihi na zenye macho kilikuwa kitu cha msaada kwa timu kwa sababu kiliihakikishia timu iweze kumiliki mpira ndani ya mchezo husika.
Hakuwa mshambuliaji halisi wa katikati lakini magoli yake yalifanikisha Simba kupata alama tatu muhimu.
Nyimbo yake ilikolea zaidi kipindi alipokuwa anatengeneza magoli kwenye mchezo husika.
Kitu ambacho kilimfanya awe mchezaji muhimu na nguzo kwenye kikosi cha mwalimu Joseph Omog.
Msimu jana ulipita na nyakati za furaha kwa Mohamed Ibrahimu, lakini msimu huu zimekuja na nyakati ngumu sana kwake.
Nyakati ambazo zinamfanya kuwa mchezaji ambaye hajapata mechi nyingi msimu huu kwa sababu mbalimbali kama majeraha na kutokuwa chagua la kocha.
Siyo jambo la kushangaza kutokuona jina lake kwenye kikosi cha Simba msimu huu.
Maisha yamebadilika kwake, kimbuga kikali kimeelekea upande wake, anahitaji nguvu kubwa kukabiliana na kimbuga hicho.
Nguvu ambayo itasaidia kuokoa kipaji chake, kipaji ambacho wengi walitamani kukiona kikifika mbali na kusaidia Taifa kwa ujumla.
Mwanga taratibu unaanza kufifia na kulikaribisha giza katika maisha yake ya mpira.
Anahitajika mtu wa kumwekea mwanga ili aweze kuona ni wapi anapotakiwa kwenda ili afike alipokuwa anapatamani siku zote.
Najua anapitia nyakati ngumu, nyakati ambazo bila kukaa na mtu wa karibu wa kumshauri vizuri kuna hatari kubwa ya ƙkumpoteza.
Anatakiwa kupokea hali halisi anayoipitia kwa sasa, aambiwe ni kawaida kwa mwanadamu kupitia nyakati ngumu kwa sababu maisha siku zote ili yakamilike yanahitaji pande zote mbili ( upande wa furaha na huzuni)
Pande hizo mwanadamu kaumbiwa, na ni lazima mwanadamu azipitie lakini kinachowatofautisha wengi ni uimara wa kupita katika nyakati ngumu.
Hakuna kipindi ambacho Mohamed Ibrahim anatakiwa kuwa imara kama kipindi hiki.
Anatakiwa kuwa na nguvu za ziada na mawazo chanya katika akili yake yatakayomwezesha ajijenge yeye kama yeye.
Mawazo chanya ambayo yatampa imani kesho imeumbwa kwa akili yake na asichoke kuisubiri kesho yake.
Naamini kwenye kipaji chake , naamini anauwezo mkubwa wa kurudi sehemu ambayo tutamsifu na kumwandika sana kwa kiwango chake bora.
Roho ya kukata tamaa haitakiwi kuwepo na kutawala akili yake, yeye ni dhahabu inayopita kwenye moto kwa sasa, thamani yake ni kubwa mno siku moto huo utakapozima
Anatakiwa kuvumilia kila kitu kibaya kinachokuja kwake, hakuna baya lisilo na faida. Mabaya humfanya binadamu awe imara zaidi.
Huwezi kuwa imara bila kupitia nyakati ngumu katika maisha yako. Hili ni suala la muda tu, aupe nafasi muda utatoa majibu sahihi kuhusu maisha yake ya mpira.
Sehemu ambayo ndiyo anaitegemea katika maisha yake.
Huu ndiyo wakati ambao masikio yake yanahitaji pamba, na kukimbia kuelekea mbele bila kumsikiliza mtu cha muhimu ajue ni wapi amepanga kwenda.
Afanye mazoezi kwa bidii, ajitume zaidi. Ajitunze vizuri kuanzia kwenye mlo mpaka muda wa kupumzika, na kila anapoamka awe na hasira ya kufika juu kupitia mazoezi ya timu na mazoezi yake binafsi, kwa kufanya hivo kesho itakuwa yake na ataimiliki yeye pekee kwa uweza wa MUNGU.