Jonas Mkude amejiunga na Yanga SC. Hujakosea kusoma. Narudia tena. Jonas Mkude amejiunga na Yanga SC.
Shusha pumzi zako kwanza. Shusha kidogo. Shusha tena. Tena. Moja ya Kaburi lililotikisika jana usiku pale Kinondoni Makaburini ni Kaburi la Mzee mmoja mtata. Anaitwa Mzee Masharubu.
Nitakupa mikasa ya huyu mzee (Babu yake na Jonas) Mzee Masharubu ni Simba kweli kweli. Kuna mambo mawili yametokea Mzee Masharubu akiwa amelala zake kaburini.
Jambo moja Jonas aliwahi kuwa mchezaji wa timu anayoipenda. Jambo la pili Jonas amejiunga na timu aliyokuwa anaichukia. Vyote viwili vimetokea akiwa hajaviona. Ni huzuni.
Sijui ingekuwaje mzee yule mtata angekuwepo zama hizi na kuyaona matukio haya mawili ya Jonas. Mzee yule nimewahi kuona akiwachapa bakola wazee wenzake kisa Simba SC.
Nyumbani kwa kina Jonas ni karibu na nyumbani kwetu pale Kinondoni. Zamani mara nyingi nilikuwa nakwenda na Jonas nyumbani kwao na kukutana na mzee yule mtata.
Nyakati zile hakukuwa na Azam TV kama ilivyo sasa. Nyumbani pale wahafidhina wa Simba SC walijazana katika Makochi na Vistuli kusubiri matangazo ya mpira katika Radio.
Wahafidhina wale ni kama vile walipageuza tawini. Walikuwa wanajaa kupiga stori za Simba SC na mtu ambaye angekwenda tofauti angekutana na mkono wa chuma wa Mzee Masharubu.
Pale nyumbani ilizungumzwa Simba SC asubuhi, mchana, jioni hadi usiku. Ni Simba SC tu. Sio kitu kingine.
Kitu pekee ninachokiamini kama Mzee Masharubu angekuwepo katika uso wa dunia Jonas angepata ukakasi kushika kalamu kuusaini mkataba wa Yanga SC. Hili nina uhakika nalo na uzuri Jonas mwenyewe analijua vizuri.
Mara kadhaa nimeona manazi wa Yanga SC wakienda kumpa zawadi za Soda Mzee Masharubu siku Yanga SC wakipata ushindi kwa Simba SC, lakini walikutana na joto ya jiwe.
Siku hiyo Mzee Masharubu angetulia na kupokea kila dhihaka ya kila neno kutoka kwa Yanga SC, uvumilivu ukimshinda anainuka kuingia ndani.
Ukiona ameinuka hapo sio sehemu salama tena. Mara nyingi manazi wale wa Yanga SC wanakimbia. Wanajua KIFUATACHO ITV.
Mungu ampumzishe Mzee Masharubu na kila la kheri Jonas Gerard Mkude.