Licha ya kutumia zaidi ya Paundi Milioni 100 kuwasajili wachezaji 12 kwenye dirisha la usajili mwaka jana lakini haijawasaidi Klabu ya soka ya Fulham kubaki ligi kuu baada ya kupanda mwaka jana.
Fulham imeshuka rasmi daraja baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Watford kwenye uwanja wa Vicarage Road usiku wa kuamkia leo licha ya michezo mitano kusalia ligi hiyo ifikie tamati.
Katika mchezo huo Fulham walikuwa wakihitaji ushindi kwa hali na mali na mpaka mapumziko walikuwa na matumaini kwani bado ubao ulikuwa ukisomeka 1-1, lakini mabao ya Will Hughes, Troy Deeney na Kiko Femenia katika kipindi cha pili yalitosha kabisa kuwaondoa kwenye ligi pendwa zaidi duniani.
Bao pekee la Fulham lilifungwa na Ryan Babel likiwa ni bao la kusawazisha baada ya Abdoulaye Doucoure kufunga bao la kwanza kwa Watford.
Kwa mantiki hiyo sasa Fulham wanaungana na Huddesfield Town kucheza ligi ya washindi msimu ujao, ikiwa ni rekodi ya kipekee kwa timu mbili kushuka daraja mapema zaidi kwenye historia ya ligi kuu England.