Mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele ameendelea kuvutia vilabu kadhaa na sasa ni nje ya Afrika kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha haswa katika michuano ya kimataifa.
Mayele mwenye mabao saba katika kombe la Shirikisho Afrika na kuifanya klabu ya Sepahan ya nchini Iran kuonyesha kuhitaji huduma ya nyota huyo Mcongo. Timu hiyo inayoshiriki Persian Galf Pro League imemaliza ligi katika nafasi ya pili na hivyo kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa ya Asia.
Awali klabu za Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundows zilionyesha nia ya kumuhitaji nyota huyo wa Yanga lakini wameonekana kurudi nyuma katika mbio hizo na kuendelea na mawindo kwa washambuliaji wengine.
Sepahan na Iran ipo tayari kutoa kiasi cha zaidi ya dola 500,000 za Kimarekani (zaidi ya bilioni 1.2 za Kitanzania) ili kupata saini ya nyota huyo wa Yanga ambae yupo katika nafasi nzuri ya kunyakua tuzo ya ufungaji bora ya Ligi Kuu ya NBC.
Kiasi hicho cha fedha kinaonekana ni kikubwa zaidi na Yanga hawawezi kukikataa lakini pia vilabu vya Afrika Kusini hawawezi kutoa kutokana na bajeti zao ndogo.
Ni wazi sasa Yanga wanapambana katika kumpata mrithi sahihi wa Mayele kuelekea msimu ujao na miongoni mwa nyota wanaotajwa na Wananchi ni mshambuliaji wa Marumo Gallanta Rango Chivaviro.