Shirikisho la soka nchini Rwanda (FERWAFA) limethibitisha kuialika Tanzania kwenye mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mashindano ambayo yatashirikisha timu tatu pekee.
Mashindano hayo yaliyopewa jina la Under 17 Mini-tournament yanatarajiwa kuanza Machi 28 na kufikia tamati April 4, 2019kwenye uwanja wa Stade de Kigali mjini Kigali, siku 10 kabla ya kuanza kwa mashindano ya Mataifa Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17).
Mbali na Tanzania na Rwanda, pia Cameroon inatarajiwa kuwa miongoni mwa timu ambazo zitashiriki kwenye mashindano hayo ambayo kwa Rwanda yatakuwa ni maalumu kwa ajili ya kujiweka fiti wakati kwa timu nyingine yatakuwa ni maalumu kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya AFCON U17 yanayotarajiwa kuanza kutimu vumbi April 14 -28, 2019 jijini Dar es Salaam.
Serengeti Boys ambayo ilishiriki mashindano ya U17-UEFA Assist wanaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kujiandaa na mashindano hayo ambapo Tanzania imepangwa kwenye kundi A wakiwa na timu za Nigeria, Uganda na Angola, ambapo itaanza kufungua dimba kwa kucheza na Nigeria saa kumi jioni.