Sambaza....

Anaitwa Feisal Salum Abdalla kiungo Wakizanzibar aliyetua ardhi ya Tanzania Bara (Bongo) mwaka 2018 kunako kikosi cha Yanga akitokea JKU ya huko Zanzibar, baada ya hapo awali Singida United kutaka sainu yake.

Kijana huyu mwenye umri wa miaka 22, Ameweza kuwaonesha Viungo wengi wa Bongo kuwa hakuja bongo kuuza sura Sinza wala Nyegezi Mwanza bali kaja kuuza bidhaa ambayo ni Ujuzi wenye kiwango chenye kuvutia wanunuzi, (Wadau wa Soka).

Ni dhahiri kuwa Tangu amejiunga na Yanga ameonesha kandanda safi chini ya waalimu wote, kuanzia Zahera mpaka sasa Luc Eymael ambapo amefanikiwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha wanajangwani hao.

Feisal Salum “Fei toto”

Sifa kuu ya Mwamba huyu ni kusoma mchezo ulivyo kwa maana ya Mechi, mzigo ukiwa mzito anaubeba kwa nguvu kubwa vivyo hivyo kazi ikiwa nyepesi anaifanya kuwa ya kuvutia zaidi, Kwa lugha ya mpira tunaweza kumuita ‘Skilled Box to box Midfielder’.

Hana mambo mengi anapokua na mpira anagusa na kuachia kwa wakati, pia timu inapokua haina mpira anafanya kila awezalo ili kuupata huku nguvu na akili vikitumika kwa kiasi kikubwa.

Kucheza timu kubwa kama Yanga kumemjenga saana kiakili na kimwili jambo lililomuweka fiti zaidi na aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kipindi hicho, Emanuel Amunike alimjumuisha kikosini na kumtumia kama mpambanaji moja wapo aliyeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afcon mwaka 2019.

Feisal Salum na mlinda mlango Menata Mchata wakiwa kambini na timu ya Taifa ya Taifa Stars.

Kwa umri na umbo lake ni ngumu kuamini kuwa ndiye anayeviweka benchi vipande vya watu kama Makame, Banka na viungo wengine kunako kikosi cha Yanga.

Sikushangaa kuona vilabu kama TP Mazembe na vingine kibao kuhitaji saini ya kiungo huyu,Bali niliona wivu kwa mauzo yake hapo baadae kama ataendelea kuwa na nidhamu, uwezo na ufundi uliotukuka na ubora zaidi maana umri wake bado unaruhusu aina zote za pesa katika mauzo, kiufupi ni bidhaa inayouzika.

Mwisho, Kila lakheri mzee baba Soka ndio ajira yako, Piga kazi macho mengi yanakutizama, nakuona mbali zaidi ya hapo ulipo sasa, Na pia wewe ni funzo kwa Viungo wengi waliopo Tanzania.

Sambaza....